BEKI wa Yanga, Mghana Lamine Moro amfungiwa michezo mitatu na kulipa faini ya Sh. 500,000, kwa kosa la kumrukia mgongoni mchezaji wa JKT Tanzania, Mwinyi Kazimoto, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara, uliochezwa tarehe 17 Juni, 2020. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).
Mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma, na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Baada ya mchezo huo kumalizika mchezaji huyo aliomba radhi mashabiki, Kazimoto pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kosa alilolifanya.
Pamoja na kufanya hivyo kamati hiyo iliamua kumchukulia hatua kwa kuzingatia kanuni ya 38(3) ya ligi kuu inayohusu udhibiti wa wachezaji.

Maamuzi hayo yametolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (kamati ya saa 72) kwenye kikao chake kilichofanyika tarehe 23 Juni, 2020.
Ikumbukwe kabla ya adhabu hiyo uongozi wa klabu ya Yanga, ulimchukulia hatua mchezaji wake kwa kumkata Sh. 1,000,000 kwa kufanya kosa hilo.
Mpaka sasa mchezaji huyo ameshakosa michezo miwili ya Ligi kuu dhidi ya Azam FC na Namungo FC ambapo klabu ya Yanga imeambulia pointi moja kwenye kila mchezo.
Aidha kamati hiyo pia imemfungia mchezaji wa JKT Tanzania, Mwinyi Kazimoto kwa kukosa michezo miwili baada ya kuleta vurugu uwanjani wakati wa mchezo huo.
Leave a comment