August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bodaboda wampinga Kamanda Sirro

Simon Sirro, Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi ya Dar es Salaam

Spread the love

WAENDESHA pikipiki ‘bodaboda’ jijini Dar es Salaam, wamepinga ushauri wa Kamanda wa Kanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, wa kufunga kazi zao kabla ya sita usiku ili kudhibiti uharifu, wanaandika Waandishi Wetu.

Kamanda Sirro alitoa ushauri huo hivi karibuni kwa kuwataka waendesha bodaboda kufunga kazi zao muda huo ili kutowapa nafasi waharifu wanaotumia pikipiki kujichanganya nao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na MwanaHALISI Online, madereva hao wamesema uharifu unaweza kuthibitiwa kwa mbinu nyingine hata kama wao wakiendelea na kutoa huduma zao, na pia unaweza kuendelea hata kama wao wakifunga kazi muda huo uliotakiwa na Kamanda Sirro.

Nurudin Hassan, Mwenyekiti wa Chama cha Bodaboda Temeke, amesema kuwa bodaboda wote wamesajiliwa majina yao yapo serikali za mitaa na polisi, hivyo ni rahisi kuwagundua kama watafanya uharifu.

Kwa upande wake, Amir Bakari wa kijiwe cha Chihita Msikitini, Tandika, amesema kuwa usafiri wa bodaboda ni salama kwa sababu wao kwa asilimia kubwa huwasaidia watu wanaorudi usiku kwani huwafikisha hadi majumbani, kinyume na hapo wanaweza kukabwa na vibaka.

“Usiku ndiyo muda wa kazi, kwani tuna abiria maalum ambao muda wao wa kurudi ni usiku. Umbali ambao mtu anapanda bodaboda usiku mchana anatembea kwa miguu, kutupangia muda ni kutukosesha kazi,”amesema Bakari.

Shabani Juma, dereva wa bodaboda katika kituo cha Manyanya,Kinondoni amesema ushauri wa Kamishna Sirro halitaweza kuondoa tatizo la wizi moja kwa moja kutokana na waanaoshiriki wizi kutokuwa na muda maalum wa kufanya uhalifu.

“Wizi wa pikipiki unaweza ukaibiwa muda wowote, naona haitasaidia chochote kwa sababu bodaboda unaweza ukasema ufanye kazi mpaka saa sita lakini unaweza ukaibiwa ndani ya masaa hayo wezi wapo haijalishi mchana au usiku,”

Madereva katika kituo hicho wameitaka serikali hususan Jeshi la Polisi kuwa na doria na kuhakikisha wanashirikiana vyema kusimamia usalama wa watu usiku kwa kushirikiana na wananchi.

“Nashangaa, doria inafanyika usiku, lakini bado matukio hayaishi. Bodaboda ni huduma ya kijamii kama zilivyo taxi naweza kutoka safari mkoani nikafika ubungo nikiwa nimechelewa nashindwa hata kulala kituoni nalazimika kutafuta usafiri wa haraka na wa bei nafuu kuliko kutafuta taxi usiku ni bei juu, hivyo ikiwa mwisho saa sita itakua ngumu kupata usafiri,” ameeleza mmoja wa abiria wa Bodaboda aliyejitambulisha kwa jina moja la Mussa.

error: Content is protected !!