SHIRIKA lisilo la kiserikali la Foundation For Civil Society (FSC) kesho linatarajia kuzindua kampeni ya “Chungulia Fursa Boda to Bado,” anaandika Victoria Chance.
Akizungumza na MwanaHALISI Online, Boniphace Makene, Afisa Mawasiliano wa shirika hilo, amesema “ lengo la kampeni hii ni kuwahamasisha vijana na wanawake kuzitambua fursa za kibiashara na uchumi zilizopo kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.”
“Kampeni zitazinduliwa na Balozi Dk. Augustine Mahinga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na tunatarajia kupata washiriki kutoka taasisi 150 ambazo tunafadhili shughuli zao,” amesema Makene.
Makene amesema mbali na kampeni hizo kuzinduliwa jijini Dar es Salaam pia zitaendeshwa katika majiji ya Arusha na Mwanza kwa kuwa ndiyo maeneo makuu ya kibiashara.
“Mafunzo yatakayotolewa kupitia kampeni hii wafanyabiashara wadogo wataongezewa kujiamini na kuwafungua macho kwenye fursa mbalimbali za biashara zinazofanywa katika mipaka ya nchi yetu,” amesema Makene.
Katika kampeni hiyo wamewaalika wafanyabiashara wakubwa kwa lengo la kuwapa changamoto wafanyabiashara wadogo kwa kuwaelezea njia walizopitia mpaka kufikia mafanikio.
Leave a comment