August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Boda boda waongoza kuwapa mimba ‘madenti’ Dodoma

Usafiri wa Bodaboda Dodoma

Spread the love

WANAFUNZI  23  wa kike katika shule mbalimbali  za msingi na
sekondari wilayani Mpwapwa, Dodoma wameshindwa kuendelea na masomo baada ya kupata ujauzito kati ya Janauri  hadi  Desemba mwaka huu, huku waendesha pikipiki maarufu kama boda boda wakitajwa kuhusika, anaandika Dany Tibason.

Jabir Shakimweri, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa ametoa taarifa hiyo katika mkutano na vijana wa boda boda wilayani hapa ambapo aliwaonya vijana hao kutoshiriki vitendo vya ngono na wanafunzi  wa kike akisema ni kosa la jinai na ni ubakaji.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Hussen   Mdoe Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mpwapwa (OCD),  vijana hawa walitakiwa kujali maisha yao ikiwemo kujiepusha na makosa yanayoweza kusababisha wakafungwa au kupoteza uhai.

“Vitendo vya ngono na wanafunzi havikubaliki, serikali haitavivumilia na ni vyema mkajiepusha navyo kwani taarifa zinaonesha bodaboda wanaongoza kwa kushiriki vitendo hivyo na wanafunzi na hivyo kukatisha masomo yao,” amesema Shakimweri.

Vijana hao pia wametakiwa  kufuata  sheria za usalama barabarani  ili kuweza kupunguza ajali katika kipindi cha mwisho wa mwaka.

“Kuanzia mwezi Januari  hadi Desemba  ajali  12 zilitokea hapa Mpwapwa ambapo ajali nane zilisababisha vifo  na ajali nne zilisababisha  majeruhi na ulemavu,” amesema OCD Mdoe.

Amesema Mpwapwa nzima  ina pikipiki  76,024 wakati vijana wanaofanya   biasahara  ya boda boda   wenye leseni  ni 200 tu hivyo amewataka  vijana hao kujiunga katika vikundi  ili kuweza kupata mafunzo  ya udreva ambayo yataratibiwa na Jeshi la Polisi.

“Na tunawaomba boda boda muwe rafiki wa polisi, mkipata taarifa za uhalifu mtujulishe ili tuweze kuimarisha usalama na amani ndani ya wilaya yetu,” amesema OCD Mdoe.

error: Content is protected !!