August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bobali: Lipumba usikanyage mikoa ya Kusini

Spread the love

JUMUIYA ya Vijana ya Chama cha  CUF (JUVICUF), Profesa Ibrahim Lipumba kutothubutu kufanya ziara katika mikoa ya Kusini kwani atajikuta akidhalilishwa na kuendelea kukosa heshima zaidi katika jamii, anaandika Charles William.

Prof. Lipumba ni Mwenyekiti wa CUF anayetambulika na Msajili wa Vyama Vya Siasa hapa nchini, ingawa tayari chama hicho kimetangaza kumfukuza uanachama kwa tuhuma za kufanya vitendo vilivyo kinyume na Katiba ya CUF.

Hamidu Bobali, Mwenyekiti wa JUVICUF Taifa ambaye pia ni Mbunge wa Mchinga, amesema vijana wa CUF hawatakubali Prof. Lipumba na wapambe wake wajaribu kuzunguka katika mikoa mbalimbali ikiwemo Lindi na Mtwara ili kukivuruga chama hicho.

Mbele ya wanahabari leo, jijini Dar es Salaam, Bobali ameeleza kuwa Jumuiya ya Vijana wa chama hicho (JUVICUF), inaunga mkono maamuzi yote halali yaliyotolewa na mamlaka halali za chama ambalo ni Baraza kuu la Uongozi la Taifa  ikiwemo ya kusimamishwa na kuwafukuza baadhi ya wanachama wake 11 ambao wanaenda kinyume na taratibu za chama.

‘’CUF ni chama cha kupigania haki hivyo abadani hakitayumbishwa na njama mbalimbali zinazoendelea za kutaka kututoa nje ya ajenda za kudai haki, pia ni taasisi kubwa ambayo inaamini katika jitihada za kudai haki. Wakati njama za kutuhujumu zikiendelea, jitihada za kudai haki zanzibar, zimefikia sehemu nzuri na baadhi ya ushahidi jamii imeanza kushuhudia,’’ ameeleza Bobali.

Bobali amewataka vijana wote wa CUF nchini, kutotoa ushirikiano wowote kwa maadui wa chama ambao wanatarajia kuanza ziara wiki ijayo katika mikoa ya Kusini, Lindi, Mtwara na Tanga katika lengo lilelile la kuweka mpasuko ndani ya chama.

“Wana lengo la kukivuruga na kukidhoofisha chama na wanataka kuvuruga ushirikiano na vyama vingine vya Ukawa, sisi kama vijana tupo imara, hatutaruhusu hilo litokee, tutawakabili na kwa hakika hawatofanikiwa katika hilo,” amesisitiza Bobali.

Naibu Katibu wa JUVICUF ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia amesema Abdul Kambaya, aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano kwa Umma kabla ya kusimamishwa uongozi katika chama hicho, ndiye anayeongoza zoezi la kuchochea vijana wakipinge chama kutokana na kukosa nafasi ya kugombea ubunge wa jimbo la Kinondoni analoliongoza baada ya kumuangusha katika kura za maoni Julai mwaka jana.

Kwa upande wake Juma Kombo, Mbunge wa Jimbo la Wingwi,  Pemba ambaye pia ni Afisa Haki za Binadamu (JUVICUF), amesema CUF Zanzibar ipo imara  huku wakiwataka vijana wa Zanzibar kutoyumbishwa na watu wachache wanaotumika kukihujumu chama hicho.

error: Content is protected !!