May 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

BMT yatia mchanga ‘kitumbua cha Yanga’

Spread the love

Baraza la Michezo hapa nchini (BMT), kupitia kwa Mohammed Kiganja, Katibu Mkuu wake, limetangaza kutotambua ukodishwaji wa Klabu ya Yanga  na kusema kuwa ni kinyume na Katiba ya klabu hiyo, anaandika Kelvin Mwaipungu.

Bodi ya wadhamini ya Yanga ikiongozwa na Francis Kifukwe jana iliuweka wazi mkataba walioingia na kampuni ya Yanga Yetu Limited, iliyoundwa maalumu na Mwenyekiti wa Klabu hiyo kwa ajili ya kuingia makubaliano ya kukodi timu na nembo katika kipindi cha miaka 10.

Kiganja amesema leo kuwa, utaratibu uliofanyika kuingia makubaliano ya kukodishwa kwa klabu hiyo kati ya bodi ya wadhamini na kampuni hiyo haukufuata taratibu.

“Ili Yanga iweze kubadili jina na kuitwa, Yanga Yetu ni lazima ipite kwa msajili. Wao hawajaenda kwa msajili wanaanza kutangaza jina jipya.  Huko ni kuipinga Katiba yao,” amesema Kiganja.

Kiganja aliongezea kuwa Baraza la Michezo linatambua kuwa klabu zinataka kufanya mabadiliko kwa malengo ya kupata mafanikio BMT inabariki mafanikio hayo lakini lazima taratibu zifuatwe.

“Lazima wanachamawapate fursa ya kujadili jambo linalotaka kutokea kwenye klabu yao pamoja na kupata ufafanuzi ikiwemo kuelimishwa juu ya faida na hasara za mifumo husika,” amesema.

Ikumbukwe Yanga kupitia wanachama wao waliridhia mabadiliko hayo ya uendeshaji wa timu katika Mkutano Mkuu wa klabu hiyo, uliofanyika Agosti 6, mwaka huu katika ukumbi wa Diamond Jubilee.

Wanachama wa Yanga wote kwa kauli moja walitoka na maamuzi ya kukubali timu hiyo ikodishwe kwa Mwenyekiti wao kwa miaka 10.

error: Content is protected !!