January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Blatter atangaza ujiuzulu Fifa

Rais wa Shirikisho la Soka la KImataifa (Fifa), Sepp Blatter

Spread the love

RAIS wa Shirikisho la Kandanda Duniani (FIFA), Joseph (Sepp) Bletter, raia wa Uswisi, barani Ulaya, ametangaza rasmi kuwa atajiuzulu wadhifa huo. Anaandika Jabir Idrissa …. (endelea).

“Nitaitisha haraka mno kikao cha kujieleza. Nitakabidhi madaraka kwa rais mpya atakayechaguliwa,” amesema Blatter, katika mkutano na waandishi wa habari alioitisha ghalfa leo mchana katika jiji la Zurich, yalipo makao makuu ya shirikisho hilo.

Taarifa iliyotangazwa na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kupitia kipindi cha Dira ya Dunia, imemnukuu ofisa mwandamizi wa Shirikisho hilo aliyeko Geneva, akisema uchaguzi wa kumpata rais mpya wa FIFA “utafanyika ndani ya miezi sita ijayo.”

“Nafikiria maandalizi yanaweza kukamilika na uchaguzi kufanyika ifikapo Desemba mwaka huu… ni jambo la dharura linalohitaji kufanikishwa,” alisema ofisa huyo bila ya kutoa maelezo zaidi.

Tamko la Blatter limekuja siku sita tu tangu makachero wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), walipovamia hoteli moja ya nchini Uswisi na kuwakamata viongozi saba wa ngazi ya juu kiutendaji katika FIFA kwa tuhuma za kushiriki rushwa.

Tukio hilo lilitokea siku moja tu kabla ya uchaguzi wa rais wa FIFA. FBI walisema watendaji hao wamehusika katika uovu wa rushwa katika nyakati tofauti wakati wa maandalizi na upigaji kura wa kuchagua nchi mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2018 na 2022.

Shirikisho hilo limetoa uenyeji wa fainali za 2018 kwa Russia na 2022 kwa Qatar. Maamuzi hayo yamepokewa kwa shingo upande na wadau barani Ulaya na Marekani.

Waliokamatwa walitajwa kama watendaji walio karibu kimaamuzi na Blatter, mtawala ambaye mara tu alipochaguliwa kushika wadhifa huo kwa mara ya tano, alisema yeye, kama alivyo binadamu yeyote, hayuko mkamilifu.

Hata hivyo, alikanusha kuhusika katika kadhia iliyowakabili watendaji wa FIFA. Alisema siku zote amekuwa akisimamia kuhakikisha mchezo wa kandanda unakuwa huru usiohusisha uchafu wa aina yoyote.

FIFA ilishikilia kuendesha uchaguzi huo licha ya shinikizo nzito za mashirikisho ya Ulaya (UEFA) na Marekani (CONCACAF) kutaka uahirishwe. Alikabiliwa na wagombea wawili, mmoja akijitoa kabla ya uchaguzi, na mwingine, akijiondoa katika duru la pili baada ya kupata kura 73 dhidi ya 178 za Blatter.

Uamuzi wa Blatter umeshangaza wengi na wachambuzi wa utawala wa kandanda wanasema kwamba wanaoiona hatua hiyo kama inayoonesha mtawala huyo wa mchezo huo ameshindwa kuvumilia shutuma kali zinazoendelea kumuandama kutoka kwa wakuu wa mashirikisho ya mchezo Ulaya na Marekani.

error: Content is protected !!