May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Biteko apiga marufuku usafirishaji gesi Mbeya

Spread the love

 

WAZIRI wa Madini, Doto Biteko amepiga marufuku kusafirisha gesi ya Kampuni ya kuzalisha Gesi Asilia ya Kabon Daioksaidi ya Tol Gases Limited iliyopo wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya bila uwepo wa viongozi wa serikali. Anaripoti Mwanaharusi Abdallah, TUDARCo … (endelea).

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya wizara hiyo imesema, Biteko ametoa marufuku hiyo leo Jumatatu tarehe 16 Agosti 2021 alipotembelea kiwanda hicho kujionea shughuli wanazozifanya.

Waziri huyo amewataja maofisa wanaopaswa kuwapo kabla ya kuruhusu kusafirisha ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mbeya, Afisa wa Takukuru, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, pamoja na Afisa kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa wilaya ya Rungwe ili wafunge lakiri (Seal) kwa lengo la kudhibiti udanganyifu.

Aidha, ameiagiza kampuni hiyo kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa na wizara ya madini ikiwemo kanuni ya uchangiaji maendeleo kwa jamii, menejimenti ya kampuni ya uchimbaji madini kuwepo eneo la mgodi pamoja na kutunza taarifa za mauzo ya madini.

Amesema kuna baadhi ya taarifa za mauzo zinazoonesha kiasi cha fedha kilichouzwa gesi hiyo hazipo kwenye kumbukumbu ya vitabu vya kampuni hiyo ambapo ni kinyume na taratibu zilizowekwa na Wizara ya Madini.

Waziri Biteko ameitaka kampuni hiyo kuhakikisha menejimenti ya kampuni hiyo inakuwapo eneo la uzalishaji baada ya kugundua uongozi wote wa ngazi za juu upo jijini Dar es Salaam ambapo sheria ya madini inasema sehemu yoyote inayochimbwa madini menejimenti iwepo na takwimu zote ziwepo mgodini.

Pia, ameitaka Kampuni ya Tol Gases Limited kuhakikisha inachangia maendeleo kwa jamii katika eneo linalozunguka mgodi ili jamii ione manufaa ya Gesi iliopo katika mazingira yao.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Dk. Vicent Anney, amemshukuru Waziri Biteko kwa kufanya ziara wilayani Rungwe na kumuahidi kwamba, ofisi yake ameyapokea maelezo na atahakikisha anayafanyia kazi kama alivyo elekezwa.

“Sisi kama wilaya ya Rungwe tutahakikisha tunasimamia vizuri maelekezo yako na tunakuhakikishia kwamba, hakutakuwa na urasimu wa aina yoyote, mimi nitashirikiana na watendaji wenzangu kuhakikisha serikali inakuwa na ofisi katika kiwanda hiki ili kulinda rasilimali za nchi na kuziba uvujaji wa mapato ya Serikali,” amesema Dk. Anney.

Vilevile, Dk. Anney, ametoa agizo kwa Kampuni ya Tol Gases Limited kwenda ofisini kwake kwa lengo la kujadiliana ni namna gani na kiasi gani kiwanda hicho kitachangia maendeleo kwa jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Kampuni ya Tol Gases Limited Freddy Sarat, amesema kampuni anayoisimamia imeyapokea maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Biteko na kumuahidi kuyafanyia kazi maekezo yake yote.

Kampuni ya Tol Gases Limited inayojishughulisha na uchimbaji na uchakataji wa Gesi ya Kabon Daioksidi ilianzishwa mwaka 1982 na kuanza uzalishaji rasmi mwaka 2013 inauwezo wa kusafirisha gesi zaidi ya magari 300 yenye Tani 20 kila moja kwa mwezi ambayo inawateja ndani na nje ya nchi.

error: Content is protected !!