November 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Biteko ahamasisha kampuni kuchangia damu salama-Geita

Spread the love

WAZIRI wa Madini Dk. Doto Biteko ameyataka makampuni mbalimbali hapa nchini kuwa na desturi ya kujitoa kusaidia Uchangiaji wa Damu Salama hospitalini kama Kampuni ya Gf Truck Group ilivyofanisha uchangiaji wa damu salama Mkoani Geita. Anaripoti Paul Kayanda, Geita… (endelea).

Amesema kampuni hiyo imeunga juhudi za Serikali katika kuhakikisha kuwa Benki ya Damu salama haipungui katika Hospitali ya Mkoa wa Geita ili kumudu kuhudumia idadi ya wagonjwa wenye uhitaji wanaofika hapo kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

 

Waziri Beteko ametoa kauli hiyo jana tarehe 1 Oktoba, 2022 kwenye maonyesho ya tano ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Bombambili mkoani Geita baada ya kutembelea kwenye banda la kampuni ya Gf Truck Group.

Kampuni hiyo ilikuwa na siku maalumu jana  kuendesha zoezi la uchangiaji wa damu salama kwa kushirikiana na kitengo cha damu salama kutoka hospitali ya mkoa wa Geita.

Dk. Biteko alionesha kufurahishwa na jambo hilo ambapo alitamka kuwa Gf Truck Group wanapaswa kupongezwa kwa hatua yao ya kuendesha zoezi hilo kupitia maonyesho haya ya tano ya teknolojia ya madini na kwamba moja ya jambo ambalo serikali wanalitilia mkazo na msukumo mkubwa ni pamoja na watanzania washiriki uchangiaji wa damu salama ili kunusuru wahitaji.

“Pia serikali inataka watanzania washiriki kwenye kwenye uchumi wa madini na katika hilo kuna watu wapo kwenye kilimo, madini na wengine kwenye mifugo hao wote waone uwepo wa madini ni fursa kwao ili kukuza uchumi wao wakiwa salama,” alisema Dk. Biteko na kuongeza;

“Gf Truck tunawapongeza sana hususani kwa siku yenu ya leo umeonyesha jambo kubwa la kuchangia damu na tunawatakia kila la kheri na hapa naomba nitoe wito kwa watanzania wengine tuchangie damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya wezetu,” alisema.

Waziri huyo aliongeza kuwa Gf Truck wameonyesha mfano na hivyo makapuni mengine, Taasisi mbalimbali nchini, watu wenye utu wa kujitolea waone hali hiyo ni muhimu sana na kuongeza kuwa pamoja na kufanya maonyesho lakini kuna kitu ambacho kinagusa maisha ya watu moja kwa moja.

Kwa upande wake Meneja Mawasiliano wa Kampuni hiyo ya Gf Truck, Smart Deus akizungumza mbele ya Waziri Biteko alisema wameendesha zoezi hilo ikiwa ni kuwarudishia jamii katika kile ambacho wanakipata.

Alisema anaamini yeye pamoja na kampuni hiyo jambo ambalo wamelifanya linakwenda kuacha alama kubwa hususani kwa wananchi wa mkoa wa Geita na kutumia mwanya huo kuwaomba uwe mwendelezo wa kuchangia Damu salama kwani hospitali ya Mkoa huo inauhitaji.

Naye Mshauri wa Damu salama kutoka Hospitali ya rufaa Mkoani humo, Halima Juma alisema kuwa tangu kuaza kwa maonyesho hayo Septemba 27 mwaka huu hadi kufikia Oktaba mosi wamefanikiwa kuchangisha chupa 148 za damu.

Pia Halima alisema watu ambao wamewafikia katika kuchangia damu salama ni pamoja na madereva bodaboda, wasanii na wananchi wengine wa Mkoa wa Geita waliohamasika wapatao 75 na kati ya hao waliofanikiwa kuchangia damu ni 25 na 50 waliobaki hawakufanikiwa kutokana na sababu mbalimbali.

Aidha, alisema uhitaji wa damu salama katika Hospitali ya Rufa Mkoa wa Geita ni mkubwa ikilinganishwa na idadi kubwa ya watu wanaofika kupatiwa matibabu hospitalini hapo.

Alitumia fursa hiyo kuwashauri wananchi wa Geita na viunga vyake kuchangia damu salama kila wakati wasisubiri hadi makongamano ama warsha kwani walengwa asilimia kubwa ni watoto wadogo, akina mama wajawazito, majeruhi wa ajali mbalimbambali pamoja na wale wenye ugonjwa wa sikoseli.

error: Content is protected !!