August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bisimba aishangaa serikali

Spread the love

HELLEN Bisimba, Mkurungenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ameleza kushangazwa na serikali kushindwa kufuta Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, anaandika Pendo Omary.

Amesema, hatua ya serikali kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu kufutwa kwa vifungu vya sheria hiyo, vinavyoruhusu watoto wa kike kuolewa wakiwa chini ya umri wa miaka 18 ni ya kushangaza.

Uamuzi wa marekebisho hayo ulitolewa tarehe 8 Julai mwaka huu, chini ya Jaji Kiongozi Shaban Lila baada ya kusikiliza kesi ya msingi iliyofunguliwa na Rebeca Gyumi, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kiraia ya Msichana Initiative iliyoitaka mahakama kufuta vifungu vivyo.

Katika mahojiano na Mwanahalisi Online leo Bisimba amesema, “haiingii akilini serikali kukatia rufaa maamuzi yaliyotolewa na Mahaka Kuu. Hatukuwahi kufikiri kama serikali inaweza kukata rufaa.

“Kwa sasa watu wanafanya kazi kwa woga. Hii ni kutokana na kauli ya Rais John Magufuli ya kuhoji kwamba, kwanini serikali imekuwa ikishidwa kesi.

“Hivyo wanaamua kuchukua hatua ya kupinga. Hivyo ndivyo tunavyofikiri kwasababu hakuna hoja ya msingi ya kufanya hivyo.”

Bisimba amesema, siku za nyuma uamuzi ukitolewa na Mahakama Kuu, kilichofuata ni utekelezaji lakini Bunge lilibadilisha sheria na kutoa nafasi ya ukataji rufaa.

Ndoa za utotoni husababisha mimba za utotoni zenye kumuathiri mtoto wa kike. Kwa mfano tarehe 2 Julai 2012 Taasisi ya Tanzania Life Improvement Association (TALIA) ilitoa taarifa kwamba, kulingana na takwimu za Wizara ya Elimu, Mafunzo na Ufundi, kila mwaka wasichana 8,000 huacha masomo kutokana na mimba za utotoni.

Ripoti hiyo ilieleza kuwa, wasichana 3,000 kati yao ni watoto wa kike wanaosoma shule za msingi.

Aidha, kila mwaka asilimia 24 ya wanawake wajawazito hufa kutokana na matatizo ya uzazi na asilimia 5 hadi 6 kati yao ni watoto wa kike wenye umri chini ya miaka 18.

Kesi hiyo ni Na. 5 ya mwaka 2016 iliyopinga vifungu Na. 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 (sura ya 29 iliyorejewa mwaka 2002), vinavyotoa mwanya kwa mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 14 kwa amri ya mahakama na miaka 15 kwa ridhaa ya wazazi.

error: Content is protected !!