WINFRIDA Mandindile (17), amejinyonga kwa madai ya mzazi mwenzie kugoma kutoa fedha za matumizi ya mtoto wao mwenye umri wa mwaka mmoja. Anaripoti Mwandishi Wetu, Iringa … (endelea).
Kisa hicho kimetokea hivi karibuni mkoani Iringa, ambapo mama wa marehemu, Agnes Donald, amedai kabla ya binti yake kuchukua uamuzi wa kujinyonga alikuwa anampa malalamiko ya mwanaume huyo ambaye wote walikuwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kihesa, kwamba hataki kumhudumia mtoto wao.
Agnes alidai kuwa, mwanae alipata ujauzito akiwa kidato cha kwanza, wakati mwanaume akiwa kidato cha nne.
“Mimi nilikuwa naye jirani namfariji nikimwambia wanaume waongo na nilikuonya toka ukiwa darasa la saba, nafikiri chanzo cha kuchukua maamuzi hayo ni msigano wa yeye na mwenzake,” amedai Agnes.
Mkuu wa Kituo Kidogo cha Polisi cha Semtema, Cosmas Ngai, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema lilichangiwa na wazazi kutokuwa karibu na marehemu wakati anapitia magumu.
“Inaonekana alikosa ushauri labda angepata ushauri wa kutosha asingechukua uamuzi huo,”amesema Afande Ngai.
Leave a comment