January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bin Seif Khatibu atupwa Uzini

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Mohamed Seif Khatib

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Mohamed Seif Khatib

Spread the love

MWANASIASA mkongwe nchini, Muhammed Seif Khatibu ameangushwa katika kura za maoni za kuwania uteuzi wa kugombea ubunge, jimbo la Uzini, Mkoa wa Kusini Unguja. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Wakati matokeo hayo yakitangazwa leo, kuna taarifa za kuzuka mgogoro wa matokeo ya kura hizo kwa jimbo la Mahonda ambako Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, ameomba kugombea kiti cha uwakilishi.

Bin Seif ambaye amekuwa mbunge wa Uzini tangu mwaka 1995, ameshindwa kwa kura na mtumishi mwandamizi, Wizara ya Kilimo Zanzibar, Salum Rehani, anayetokea kijiji cha Kiboje, Wilaya ya Kati, mkoani Kusini.

Kiongozi huyo pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CC-NEC-CCM) ambaye ndiye aliyeratibu utoaji na upokeaji wa fomu kwa makada walioomba kuteuliwa kugombea urais kupitia chama hicho. Wanachama 40 walichukua fomu lakini 38 ndio walizirudisha. Tayari CCM imemteua Dk. John Magufuli, anayemaliza kuwa waziri wa ujenzi.

Rehani ni mwanasiasa mpya kwa siasa za kitaifa lakini kushinda kwake kura za maoni kunajenga historia mpya ya kijiji cha Umbuji, wilayani humo, kupokwa nafasi ya kutoa mwakilishi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Bin Seif ni mzaliwa wa kijiji hicho ambako amekuwa akilaumiwa kwa kutosimamia ipasavyo uratibu wa harakati za kupeleka maendeleo kijiji kwake hapo, lawama zinazomkabili kwa ujumla kwa vijiji vyote vya jimbo.

Tangu mwaka 2012, kulikuwa na harakati kubwa za siri kwa wana-CCM wa jimbo hilo kutaka kuona Khatibu ambaye anaungwa mkono na viongozi wa ngazi ya kitaifa mkoani na wilayani, anaondoka kuwa mbunge.

Kampeni hiyo iliimarika pale CCM ilipokuwa inatafuta mgombea uwakilishi baada ya kufariki kwa aliyekuwepo. Mohamedraza Dharamsi, mfanyabiashara maarufu Zanzibar, aliibuka mshindi na akachaguliwa kwa kura nyingi kuwa mwakilishi mpya.

Zipo tetesi kuwa Raza ndio mhimili wa kampeni dhidi ya Bin Seif, ikisemekana amewapa nguvu ya hali na mali makada waliogombania kuteuliwa kugombea ubunge naye.

Kada mwingine katika harakati hizo ni Haji Vuai Abdalla, mtaalamu wa menejimenti ya uongozi katika bahari ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa baharibi (ZMA).

Taarifa kutoka jimbo la Mahonda, zinasema Balozi Seif ameangushwa kwa kura lakini uongozi wa juu wa CCM Kisiwandui, umesema kura itarudiwa.

Hakuna maelezo zaidi ya kusema kuna taratibu zilikiukwa wakati wa uchaguzi huo.

Jimbo la Mahonda ni miongoni mwa majimbo mapya yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ambayo hata hivyo hayakukubaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inayosimamia uchaguzi wa Rais wa Tanzania, wabunge na madiwani wa halmashauri za Tanzania Bara.

Manaibu waziri wawili katika serikali ya Muungano, Mahadhi Juma Maalim na Pereira Ame Silima, ni miongoni mwa makada maarufu walioangushwa kura ya maoni upande wa Zanzibar.

Mahadhi aliyekuwa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa (jimbo la Muyuni, Wilaya ya Kusini Unguja, ambalo sasa linaitwa Paje), na Pereira aliyekuwa mambo ya ndani (jimbo la Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja), wamepoteza nafasi ya kurudi kuendelea kuwa wabunge kwa kipindi cha pili.

Ibrahim Raza, mdogo wa Raza, ameingia katika kinyang’anyiro cha ubunge baada ya kushinda kura ya maoni ya jimbo la Dimani, akimuangusha Abdalla Sharia Ame, aliyechaguliwa Oktoba 2010.

error: Content is protected !!