Tuesday , 23 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Bima ya majeneza yaanzishwa Tanzania
Habari Mchanganyiko

Bima ya majeneza yaanzishwa Tanzania

Spread the love

KWA kile kinachoonekana si jambo la kawaida kutokea katika jamii, kampuni ya huduma za mazishi ya Goodmark imeanzisha huduma ya bima ya majeneza, ambapo mteja anaweza kulipia kidogo kidogo jeneza kabla hajafariki. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kilimanjaro … (endelea).

Hii imeelezwa kurahisisha shughuli za mazishi kwa mteja atakayekuwa amelipia kabla na kuwa ndugu hawatahangaika kupata jeneza, kwani marehemu atakuwa ameshalilipia tayari enzi za uhai wake.

Lucas Gondwe, Mkurugenzi Mwenza wa Goodmark amesema huduma hiyo ni nzuri na inamfanya mtu kujiandaa mapema badala ya kufanya wanafamilia kuchangishana na kuzikwa na jeneza lisilo chaguo lake.

“Uzuri wa hii huduma unalipa kidogokidogo, kadri utakavyopata fedha, lakini unakuwa tayari umechagua aina ya jeneza unalotaka kuzikwa nalo, tofauti na kuchaguliwa wakati umeshakufa tayari,” amesema.

Kwa mujibu wa Gondwe, kampuni ina matawi maeneo tofauti tofauti na ni rahisi kama umauti ukimkuta mteja akiwa eneo lingine, anaweza kupata huduma hiyo, kwani ni haki yake na alishailipia tayari.

“Tuseme umelipia hapa makao makuu Moshi- Kilimanjaro, ila umauti ukamkuta Arusha, hapo hakuna tatizo, ndugu watakwenda kwenye ofisi zetu za Arusha na viambatanisho na kupewa jeneza, nirahisi tu mbona,” amesema.

Amesema haimzuii mteja kubadilisha aina ya jeneza atakalopendezwa nalo, kwani karibu kila mara hutoka aina mpya.

Amesema, mteja anawezakubadilisha kwa kuongeza fedha kutokana na aina atakayovutiwa nayo na akatengenezewa.

Hivi karibuni, kampuni hiyo ilitangaza kuanzisha huduma ya makaburi ya kupanga, lengo likiwa ni kusitiri wafu katika eneo salama na hii ilitokana na mkoa wa Kilimanjaro kukumbwa na uhaba wa ardhi.

Utaratibu huo unalazimisha mtu kuzikwa eneo lao na kulipia kiasi cha fedha, na baada ya muda kama wa miaka 10, wanamfukua na kuondoka na mabaki huku eneo hilo likitumika tena na mtu mwingine.

“Itakuwa ni sehemu nzuri yenye mandhari yakuvutia, ambapo ndugu wa marehemu wanaweza kuja kupumzika wakati wa mwisho wa mwaka, na kutafakari pamoja na kufanya ibada, tofauti na ilivyo kwa maeneo ya umma,” amesema Gondwe.

Mkazi wa Moshi, Paulina Mallya amesema mila na desturi za kichagga haziruhusu mtu kuongelea mambo ya kifo kukiwa hakuna msiba, hivyo biashara hiyo ya kulipia majeneza kabla, inaweza isipate wateja kwa Kilimanjaro.

“Ukizungumzia mambo ya kufa mbele za watu wenye umri, wanaona kama unajitabiria, lakini hawajui ipo siku utakufa hii biashara ina malengo mazuri, ila itachukua muda jamii kuikubali na kuielewa pia.

Ajijengea kaburi

Hivi karibuni, mganga wa tiba asili maarufu ‘dokta’ Antony Mwandulami alifariki dunia na kuzikwa kwenye kaburi alilojiandaliwa wakati akiwa hai.

Mwandulami, mkazi wa kijiji cha Itunduma, Njombe, Iringa alijenga eneo la makaburi yake na wake zake watatu, ambayo yaligharimu takriban Sh.1 bilioni.

Akizungumza na vyombo vya habari enzi za uhai wake, Mwandulami alisema ameamua kujenga kaburi hilo kwa lengo la kuweka kumbukumbu kwa jamii yake, familia na hata kazi yake ya utabibu akiwa na wake watatu na watoto 19.

Kuhusu kaburi hilo na ujenzi wake, Mwandulami alisema ni kama nyumba ya chini iliyogawanywa sehemu nne.

“Ukubwa wa kaburi langu ni ekari moja, kwani nimejenga ngome kubwa na ndani yake kuna eneo la kaburi chini ya ardhi. Eneo la kaburi ni kubwa, kwa sababu kutakuwa na maeneo tofauti,” alisema.

“Nataka kutunza kumbukumbu za kazi zangu ambazo nimezifanya kwa muda mrefu, sitaki jina langu lipotee, hivyo nataka kutengeneza kaburi la kipekee,” alifafanua.

Alisema kwenye nyumba hiyo ambayo ni kaburi, kuna makaburi manne, moja lake na mkewe mkubwa lakini pia kuna sehemu nyingine kuna kaburi la wake zake wawili.

“Kama nilivyosema awali, nataka kuacha kumbukumbu, kwa hiyo ili kufika kwenye kaburi langu, kuna sehemu ya mapokezi, na sehemu zingine za kupumzika wageni watakaotembelea kaburini ambalo liko kina cha meta 30 ardhini,” alisema.

“Ninaagiza marumaru kutoka Sweden kwa ajili ya kumalizia makaburi hayo. Hizi zitasaidia kutunza mwili wangu kwa muda mrefu ili vizazi na vizazi vinione na kujifunza kwa huduma nilizokuwa nazitoa wakati wa uhai wangu,” alijigamba.

“Watanzania wana woga sana katika kuzungumzia suala la kifo, lakini mimi na wake zangu tumezungumza na wameridhia na kubariki ujenzi huo wa kaburi letu,” alimalizia mtabibu huyo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

NMB yadhamini Mkutano Mkuu ALAT, kufunguliwa na Samia

Spread the loveBENKI ya NMB, imekabidhi hundi yenye thamani ya Sh. 120...

Habari Mchanganyiko

DC ampongeza Dk. Rose Rwakatare kwa kusaidia waathirika wa mafuriko Mlimba

Spread the loveMWENYEKITI wa Wazazi CCM Mkoa wa Morogoro, Dk.  Rose Rwakatare...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mipango na uwekezaji kutumia bilioni 121.3, mradi wa Bagamoyo wapewa kipaumbele

Spread the loveWIZARA ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, imeliomba Bunge...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mbunge ataka kasi uzalishaji walimu ipunguzwe akidai hakuna ajira

Spread the loveMBUNGE wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, ameishauri Serikali ipunguze kasi...

error: Content is protected !!