SERIKALI ya Tanzania, imetenga Sh.8.4 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa mirefeji ya maji katika maeneo ya Mbweni mkoani Dar es Salaam. Anaripoti Nasra Bakari, DMC … (endelea).
Hilo limesemwa leo Jumanne, tarehe 27 Aprili 2021, bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Tamisemi, David Silinde wakati akijibu swali la Felista Njau, Mbunge wa Viti Maalum (asiye na chama), baada ya kufukuzwa Chadema yeye pamoja na wenzake 18 akiwemo Halima Mdee.
“Je, serikali ina mkakati gani wa kutatua tatizo la mafuriko katika maeneo Mbweni, Teta, Bunju Basihaya, Kunduchi, Nyamachabes, Ununio na Mikocheni katika jimbo la Kawe,” ameuliza Njau
Akijibu swali hilo, Silinde amesema, serikali inafanya tathmini ili kuhakikisha inasaidia maeneo yote ambayo yanakubwa na mafuriko hususani jimbo la Kawe.

“Serikali ipo kazini katika kufanya tathmini ya mwisho ili kusaidia maeneo ya Mbweta, Teta, Bunju Basihaya, Kunduchi, Nyamachabes, Ununio na Mikocheni kupunguza tatizo la mafuriko katika jimbo hilo la kawe,” alisema Silinde.
Katika swali la nyongeza la Njau, ameuliza ni lini serikali itaweka mikakati madhubuti kuondoa majanga ya mafuriko hususani kwa kujenga mifereji?
Silinde amejibu swali hilo akisema, moja ya mkakati wa serikali ni kila barabara itakayojegwa kwa sasa, itaambatanishwa na ujenzi wa miundombinu ambayo ni mifereji.
“Serikali imetenga Sh.8.4 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa mfereji wa maji ya mvua yenye urefu wa kilomita 8.89, katika Kata ya Mbweni na awamu nyingine itajumuisha maeneo mengine yaliyobaki,” alisema Silinde ambaye ni Mbunge wa Tunduma (CCM).
“Vilevile wataendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya barabara, madaraja na mifereji ya maji ya mvua ili kuondoa kero ya mafuriko maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam ikiwemo jimbo la Kawe,” alisema Silinde.
Leave a comment