December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bilioni 60 zatengwa kuchangamkia fursa ya mabondo ya samaki China

Spread the love

KATIKA kuchangamkia fursa ya soko la mabondo ya samaki nchini China, Serikali imeongeza bajeti ya kiasi cha Sh bilioni 60 katika sekta ya uvuvi ili kununu boti zinazowawezesha wavuvi kuachana na uvuvi wa kutumia zana za zamani na kutumia zana za kisasa.

Katika mwaka huu wa fedha, jumla ya boti 230 hadi 240 zinatarajiwa kununuliwa na kusambazwa kwa vikundi vya wavuvi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yameelezwa leo tarehe 12 Novemba, 2022 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati akieleza namna Serikali ilivyojipanga kuchangamkia fursa hiyo ya mabondo ya samaki pamoja na soko la parachichi

Hatua hiyo imekuja baada ya kukamilika kwa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini China iliyoanza Novemba 2 hadi 4, mwaka huu kutokana na mwaliko wa Rais wa China, Xi Jinping.

Amesema mradi huo wa kuongeza zana za kisasa ni programu ya miaka mitatu ya kushughulika na sekta za uzalishaji ambapo katika mwaka ujao wa fedha zitanunuliwa 300 na kuongezeka tena mwaka mwingine wa fedha unaofuata.

Aidha, amesema kwa upande wa Zanzibar, Dk. Mwigulu amesema walinunua boti za kutosha kwa ajili ya kufufua uchumi na tayari uzalishaji wa mazao ya samaki umeongezeka Visiwani humo chini ya fedha za Uviko-19.

Kuhusu Parachichi, Dk. Mwigulu amesema wizara ya kilimo pamoja na ile ya viwanda, biashara na uwekezaji imeshaanza kuchukua hatua zipatikane mbegu bora za zao hili.

“Pia bajeti iliyopita, Serikali ilichukua hatua ya kuondoa baadhi ya kodi kwenye mazao ya parachichi na samaki kuanzia kwenye uzalishaji, uhifadhi na usafirishaji ikwemo vyumba vya ubaridi,” amesema.

Aidha, ametoa rai kwa Watanzania kuzalisha bidhaa hizo kwa kuzingatia viwango ili kufaidika na soko hilo pamoja na kutangaza bidhaa za mazao mengine yanayopatikana nchini.

Awali Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Zuhura Yunus alisema kwamba katika ziara hiyo, Rais Samia pamoja na mambo mengine alisaini mikataba 15 ikiwamo ya fursa za wakulima kuruhusiwa kuuza zao la parachichi na bidhaa za samaki hasa mabondo nchini humo.

error: Content is protected !!