Friday , 29 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Bilioni 571 kupanua kiwanda cha sukari Kilombero
Habari Mchanganyiko

Bilioni 571 kupanua kiwanda cha sukari Kilombero

Spread the love

KIASI cha shilingi bil. 571 zinatarajiwa kutumika katika upanuzi wa kiwanda cha sukari Kilombero, na kusaidia wakulima kuchakata zaidi ya tani milioni 1.5 za miwa kutoka tani 600,000 za sasa, hali itakayopelekea kuongeza uzalishaji wa sukari. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro… (endelea)

Ofisa kilimo wa wakulima wa nje kutoka Kiwanda cha Sukari Kilombero, Barka Salim alisema hayo jana kwenye banda la kilimo la Bodi ya Sukari Tanzania lililopo kwenye maonesho ya siku ya wakulima 88 kanda ya Mashariki yanayofanyika kwenye uwanja Mwalimu Julius Nyerere mkoani hapa.

Salim alisema katika upanuzi huo wa kiwanda cha K-4, Serikali itatoa kiasi cha asilimia 25 na Kiwanda (wawekezaji) asilimia 75.

Alisema wakati umefika sasa kwa wakulima kuanza kupanua mashamba na kuwa na mashamba mapya ili kuweza kutumia fursa hiyo ya Kiwanda vizuri kwa kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.

Salim alisema awali wakiwa na viwanda vya K-1 na K-2 walikuwa wanachakata tani laki 6 hadi laki 666,000 za miwa kwa msimu uliopita kutoka hekta zaidi ya 15,000 za wakulima wa nje na kampuni hekta 11,000 na hivyo kuwa na jumla ya hekta 26,000.

Alisema kiwanda hicho kipya mbali na kusaidia wakulima kuongeza uzalishaji na kupata mauzo lakini pia kitasaidia kuondoa kero mbalimbali ikiwemo ya mabaki wanayotumia kuzalisha umeme wao (baggers) kwa kuzuia yasitoke nje na kusumbua jamii.

Nao wakulima wa miwa wa Mtibwa Wilayani Mvomero mkoani hapa wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kutoa bei elekezi ya mauzo ya miwa viwandani ili waweze kunufaika na kilimo hicho kama wanavyonufaika wenzao wa Kilombero.

Mmoja wa wakulima hao Ally Mayogo alisema jana kuwa wakiwa wakulima wa miwa wa muda mrefu wamekuwa wakiuza miwa kiwandani Mtibwa kwa bei ya sh 70,000 kwa tani tofauti na Kilombero ambao wamekuwa wakiuza kwa sh laki 120,000 kwa tani.

Naye mkulima mdogo wa miwa kutoka Kilombero Bakari Mkangamo aliwataka wakulima kujikita kwenye kilimo cha miwa kwa sababu kimemtoa kwenye hatua moja kwenda nyingine na kumfanya amiliki nyumba mbili, kupeleka shule watoto na kuendesha familia yake vizuri.

Mkangamo aliwashauri wakulima kujiunga na kilimo hasa wa kilombero sababu kwa sasa kiwanda kinapanuliwa na baada ya upanuzi huo tani nyingi za miwa zitahitajika ambapo alisema kilimo cha miwa hakina usumbufu wa kutaka mkulima kufika shambani mara kwa mara.

Hata hivyo, aliwataka wakulima kutumia teknolojia ya kisasa ya dron katika umwagaji dawa na mbolea ili kuondokana na athari za madawa kwa binadamu ikiwemo baadhi ya wakulima kuathiriwa na dawa hadi kufikia kupoteza maisha na kwamba teknolojia hiyo itapunguza athari hizo.

Naye mkulima wa miwa Mkulazi Edward Kasubi aliwashauri wakulima wengine nchini kujiunga na kilimo cha miwa kwani kilimo hicho kina tija isiyoelezeka ambayo wakulima itawanufaisha katika kuleta maendeleo yao na nchi kwa ujumla.

Kasubi ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha ushirika wa miwa katika chama cha wakulima wa miwa Magole aliwashauri wakulima wakitaka kutajirika bila kuiba waingie kwenye kilimo cha miwa kwa sababu kina faida ambapo alifafanua kuwa heka moja kuanzia kupanda hadi kuvuna inagharimu sh. Mil 1.2 hadi Mil 1.6 na kupata faida ya Mil 2.5 baada ya siku 45.

Alisema wakulima wengi wanapata tani 40 hadi 80 na wao wamejiwekea lengo la chini kuwa ni kupata tani 45 na kwamba mkulima akimaliza taratibu zote za kukata, kusomba, kupakia hadi kushusha kiwandani atajua amepata kiasi gani cha fedha sababu kilimo hicho pia hakina wizi.

Hivyo alisema kuhudumia vizuri mashamba kutasaidia kupata tani nyingi za muwa na mkulima mmoja mmoja kunufaika na Serikali kuondoa upungufu wa sukari uliopo nchini.

Aidha, Kasubi alisema akiwa mkulima mwenye kulima heka 78 za miwa atawashawishi wakulima wenzie kutoka katika zama za zamani na kuingia zama za  kisasa kwa kutumia kampuni za kumwaga dawa na mbolea kwenye mimea kwa teknolojia ya dron.

Alisema matumizi ya kawaida ya umwagaji dawa na mbolea mashambani husababisha upotevu wa mbolea na dawa sambamba na kuwa wanapoteza muda mwingi kwa zoezi hilo ambapo kwa solo la kawaida hutumia hata masaa 6 kwa heka 10 lakini kwa kutumia dron muda huwa ni mchache usizidi nusu saa kuwafanya kupata muda wa kufanya shughuli zao zingine.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya umwagaji dawa na mbolea kwenye mashamba ijulikanayo kama ELLYGREENTECH, Elibariki Nsenuka aliwataka wakulima kuitumia vizuri fursa hiyo ya dron, kwani haina gharama kubwa na utumia muda mfupi tofauti na ubebaji wa solo.

Nsenuka alisema alianzisha kampuni hiyo baada ya kuona wakulima wanapata tabu katika kukamilisha majukumu yao ya shambani katika umwagaji dawa na mbolea kutokana na gharama zilizopo iwapo mkulima atatumia ndege.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Mtandao watetezi wa haki za mazingira Tanzania waundwa

Spread the loveMTANDAO wa watetezi wa haki za mazingira nchini Tanzania, umeundwa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga kuongoza usambazaji wa mitungi ya gesi 10,000 ya Taifa Gas

Spread the loveNaibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameahidi kuongoza kwa ufanisi...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wafanyabiashara, wawekezaji China waridhia kuwekeza bil. 800 katika sekta 5 nchini

Spread the loveUJUMBE wa wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa kutoka Jimbo la Changzhou...

Habari Mchanganyiko

Bil. 4.42 kumaliza uhaba maji kata 2 Musoma Vijijini

Spread the loveWANANCHI wa kata za Busambara na Kiriba, Jimbo la Musoma...

error: Content is protected !!