May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bilioni 57 kuboresha hospitali za rufaa Tanzania

Dk. Godwin Mollel, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Spread the love

 

SERIKALI imetenga Sh.57 Bilioni kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya Hospitali za Rufaa za Mikoa, ikiwemo ya Mawenzi, mkoani Kilimanjaro. Anaripoti Jemima Samwel DMC … (endeelea).

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa, tarehe 23 Aprili 2021, bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Godwin Mollel wakati akijibu swali la Zuena Bushiri wa Viti Maalum.

“Je, ni lini jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Mawenzi litakamilika na kuanza kutoa huduma stahiki,” amehoji Bushiri.

Akijibu swali hilo, Dk. Mollel amesema, wizara inaendelea na ujenzi wa jengo la kuwahudumia mama na mtoto, ambalo kwa sasa limefikia asilimia 70.

“Mradi huo unagharimu jumla ya Sh.10.5 Bilioni ambayo hadi sasa kiasi cha Sh.5.3 Bilioni kimetolewa na kutumika,” amesema Dk. Mollel

“Katika mwaka wa fedha 2021/22, Serikali imetenga kiasi cha Sh.57. Bilioni kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya Hospitali ya Rufaa za Mikoa, na ikiwemo Mawenzi ambayo imetengewa Sh.3.6 Bilioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na Sh.1.6 Bilioni kwa ajili ya vifaa tiba,” amesema.

Aidha Dk. Mollel amesema, huduma zitaanza kutolewa baada ya kukamilika kwa ujenzi na usimikaji wa vifaa ifikapo Januari 2022.

error: Content is protected !!