May 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Bilioni 3 za Benki ya Dunia kujenga machinjio ya kisasa Dodoma

Spread the love

BENKI ya Dunia (WB), inatarajia kutoa kiasi cha Sh.3 bilioni kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa machinjio tatu za kisasa jijini Dodoma. Anaripoti Danson Kaijage…(endelea).

Fedha hizo ambazo zitatolewa na WB kupitia mradi wake wa Tanzania Cities Transforming Infrastructure and Competitiveness (TACTIC), unatarajiwa kuanza katikati ya mwaka huu.

Ujenzi wa machinjio hayo, utafanyika katika maeneo ya Nala, Msalato na Nzuguni.

Mbali na kuboresha utoaji wa huduma katika sekta ya nyama ndani ya jiji la Dodoma, machinjio hayo ya kisasa, yanatarajia kuvutia masoko ya nyama ya nje ya nchi, haswa kutoka Misri, Iran, Saudi Arabia na nchi zingine za Emirates.

Mratibu wa mradi wa TACTIC, katika halmashauri ya jiji la Dodoma, Mhandisi Emmanuel Manyanga amesema machinjio hayo yatajengwa katika viwango vya kimataifa.

“Mradi huu, unakuja kufuatia utekelezaji mzuri wa Mradi wa Miji Mkakati wa Tanzania (TSCP) ambao ulitekelezwa katika mkoa wa Dodoma kwa miaka kumi iliyopita (2011-2020), kupitia fedha kutoka Benki ya Dunia (IDA Credit) na ruzuku kutoka kwa Serikali ya Ufalme wa Denmark, kwa kiasi cha Sh.147 bilioni,” amesema

“Benki ya Dunia, imeridhishwa na namna ambavyo fedha za utekelezaji wa miradi yake Jijini Dodoma zimetumika kwa uzalendo na uaminifu mkubwa hivyo wameridhia kuendelea kutupa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mingine,” amesema Manyanga

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dk Gratian Mwesiga amesema, machinjio ya Msalato yatatengenezwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 1,000 na mbuzi 500 kwa siku ambapo machinjio ya Nala na Nzuguni kila moja yatakuwa na uwezo wa kuchinja Ng’ombe 100 na mbuzi 500.

Alisema uwekezaji huo pia utahusisha kuanzishwa kwa mahali ambapo ng’ombe zitakusanywa na kuhifadhiwa kwa angalau masaa nane hadi kumi na mbili kabla ya kuchinjwa, kama inavyotakiwa kwa mujibu wa viwango vya kimataifa.

Utekelezaji wa ujenzi wa machinjio hayo ya kisasa kutalifanya Jiji la Dodoma kuwa kitovu cha huduma bora za nyama kufuatia uwepo wa kampuni inayoongoza ya nyama nchini, Tanzania Meat Company Tanzania (TMC).

Machinjio ya TMC yalijengwa na serikali kati ya 2002 na 2003 na yalianza kufanya kazi mnamo mwaka 2004. Kurugenzi ya Mradi wa Masoko ya Mifugo Tanzania katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilisimamia ujenzi wa machinjio hayo.

Machinjio hayo yaliyopo eneo la Kizota jijini Dodoma yanauwezo wa kuchinja ng’ombe 200 na mbuzi 1,200 kwa siku, wakati mahitaji halisi kwa siku ni zaidi ya ng’ombe 600 na mbuzi 2,800 kwa siku.

Tanzania inashika nafasi ya pili baada ya nchi jirani ya Kenya kati ya nchi za Afrika Mashariki na uzalishaji mzuri na tija ya nyama pamoja na masoko ya nje.

error: Content is protected !!