JUMLA ya Sh bilioni 120.7 zimetumiwa na Halmshauri ya Jiji Ilala katika uboreshaji wa miundombinu ikiwamo ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 41 na ujenzi wa masoko matatu ikiwa ni utekelezaji wa Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP). Anaripoti Gabriel Mushi, Dar es Salaam …(endelea).
Mradi huo uliopo chini ya usimamizi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), umewezesha ujenzi wa masoko matatu, ununuzi magari matano ya taka pamoja na kontena 15 za kukusanyia taka hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana tarehe 1 Februari jijini Dar es salaam, Mraribu Msaidizi wa miradi ya DMDP kwa upande wa Ilala, Mhandisi Celestine Rwegasira amesema fedha hizo ni sehemu ya Sh bilioni 600 ambazo ni fedha za DMDP kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
Amesema katika utekelezaji wa mradi huo, pia wamefanikiwa kutengeneza visima 10 vya maji, vyoo vya umma vitatu ambavyo vimejenga kwenye shule na zahanati ya Kiwalani.
“Pia tumejenga maeneo ya bustani za kisasa kupumzikia wananchi katika eneo Yombo na Kiwalani. (Community park),” amesema.
Amesema lengo la mradi huo ni kupunguza msongamano magari mijini na kuwaleta watu kwenye ukanda wa barabara za mwendokasi.

Ameongeza kuwa lengo linguine ni kuwatoa watu kwenye maeneo ya ndani kuja mijini na kuboresha makazi holela.
Ametaja barabara zilizojengwa kuwa pamoja na Omar Londo, Kiungani, Ndanda, Olimpio, Maji Chumvi na Kilungule inayounganisha Ilala na Wilaya ya Kinondoni kuelekea Kimara Korogwe.
Nyingine ni Ulongoni Kilitex inayokwenda hadi Bangulo Kinyerezi kilometa 7.5 ambazo zote zimeleta mabadiliko makubwa kwenye makazi ya wananchi na kupunguza msongamano.
Aidha, amesema wamejenga mifereji ya kilometa 16 iliyopunguza changamoto ya mafuriko yaliyokuwa yakisumbua wananchi.
Amesema wakati wa utekelezaji huo, walilazimika kulipa fidia kwa wananchi ya Sh bilioni 11.9, ambapo Serikali imetoa Sh bilioni tisa na Sh bilioni 2.9 zilitolewa na halmashauri ya manispaa hiyo.

Kuhusu ujenzi wa bustani ya kupumzikia ya Ulongoni, Mhandisi Rwegasira amesema ni miongoni mwa bustani nne zilizojengwa ikiwa na maeneo ya kupumzikia na uwanja wa mpira wa miguu.
“Bustani hii ni kwa ajili ya wananchi kupumzika bure kabisa, kuna uwanja wa michezo.
“Awali daraja hili halikuwepo kwenye mpango, lakini kutokana na mvua za mwaka 2019 zilisomba daraja lililokiwepo, hivyo tukaongeza bajeti ili kujenga daraja,” amesema.
Amesema gharama ya mradi huo ambayo imejumuisha barabara za maungio, bustani na daraja ni Sh bilioni 6.6.
WANANCHI WANENA
Aidha, Mwenyekiti wa mtaa sa Ulongoni A kata ya Gongolamboto, Abdulrahim Munisi amesema mradi huo umekuwa fursa kubwa kwa wananchi.
“Kabla ya daraka, kulikiwa na changamoto kubwa, vifo vilikwepo kitokana na mafuriko. Watu walikuwa wamejenga kando ya mto na nyumba zilipelekwa na mafuriko.
“Lakini sasa tunaishukuru serikali kwa mradi huu ambao sasa umeboresha. Tutakuwa na kamati ndogo ya kusimamia uwanja huu na eneo la mapunziko,” amesema.
Mmoja wa wananchi wa eneo hilo la Ulongoni A, Veronica Ndege amesema awali mvua ziliponyesha walikuwa wanapata adha kubwa ikiwa ni pamoja na ukosefu wa usalama kwani wahalifu walitumia maeneo hayo kukaba watu.
Naye Mbegu Daudi amesema kuwa kabla ya barabara hiyo kujengwa kwa kiwango cha lami walikuwa wanapata shida hususani wanafunzi waliokuwa wanavuka katika daraja hilo kuelekea shule.
“Kutokana na ujio wa miradi hii kwa jamii yetu, natoa wito kwa wananchi wenzangu hususani madereva bodaboda kuheshimu alama za usalama barabara ili kupunguza ajali lakini pia wananchi tuilinde miundombinu hii,” amesema.
Leave a comment