July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bila Tanganyika, hakuna Zanzibar yenye mamlaka kamili

Utiaji saini Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Spread the love

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeamua kufia kwenye hoja yake ya muundo wa Muungano wa serikali mbili.

Vikao vya juu vya chama hicho – Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Kamati (CC) – vilivyofanyika mwezi uliopita mjini Dodoma, vimesisitiza umuhimu wa kuendelea na Muungano wa serikali mbili kwa madai kuwa hiyo ndiyo sera ya chama hicho.

Hata andishi la CCM, lililowasilishwa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, limepinga mapendekezo ya kuwapo kwa serikali tatu ndani ya Jamhuri ya Muungano.

Andishi limesema, mwarobaini wa matatizo ya Muungano, siyo kuwapo kwa serikali tatu bali serikali mbili.

Katika kutetea mfumo wa serikali mbili, chama hicho kimejikita kwenye hoja kubwa tatu:

Kwanza, muundo wa Muungano wa serikali tatu ni kinyume cha makubaliano yaliyofikiwa Aprili 1964 na waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume.

Pili, Muungano wa serikali tatu utaongeza gharama serikalini; utaingiza nchi kwenye umasikini na utasababisha Zanzibar kushindwa kuchangia uendeshaji wa serikali ya pamoja. Hoja inayojengwa ni kwamba mapato ya Zanzibar ni madogo ukilinganisha na Tanganyika.

Tatu, mfumo wa Muungano wa serikali tatu, siyo sera ya chama hicho tawala. Kinasema sera ya CCM ni serikali mbili kuelekea serikali moja. Inadai kuwa mfumo wa serikali tatu unahatarisha uhai wa Muungano.

Ukichunguza hoja hizi za kupinga Muungano wa serikali tatu na utetezi kwenye serikali mbili, waweza kuona jinsi chama hiki kinavyozeeka kwa kasi; kinavyoshindwa kufikiri, kuchambua na kutafiti.

Kwa mfano, kinachoelezwa na CCM kuwa “…umuhimu wa kuendeleza mfumo wa serikali mbili,” hakichambui madhira yaliosababishwa na mfumo huo kwa miaka 49 iliyopita; au madhara yake katika siku zijazo.

Hakijielekezi kutafuta njia mbadala ya kutatua matatizo yaliyopo; wala jinsi ya kupata suluhu ya manung’uniko ya washirika wa Muungano.

Hoja zote za chama hiki zinaishia kwenye kauli rejareja za ukubwa wa gharama; taifa kurudi nyuma; hofu ya kuvunjika kwa Muungano na inachoita, “kinyume na makubaliano ya waasisi wa Muungano wa mwaka 1964.” Basi!

Nani amekiambia chama hiki lini kulianza kuwa Muungano ni suala la sera za vyama? Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulifungwa mwaka 1964. Vyama vya Afro Shirazi Party (ASP) Tanganyika African National Union (TANU) viliungana mwaka 1977 – miaka 13 baada ya Muungano.

Wala Muungano hauwezi kudumu kwa kisingizio cha sera ya chama. Waweza kudumu kwa wananchi kukubaliana kwenye muundo na mfumo. Utadumu kwa kukubaliana kipi kiwe cha Muungano na kipi kiondoke.

Muungano hauwezi kuvunjika kwa kubariki mfumo wa serikali tatu. Utaweza kuvunjika ikiwa CCM itawalazimisha wananchi kuwa watumwa wa kubakia kwenye serikali mbili.

Nani asiyejua kuwa kauli za viongozi Visiwani za “…tunaminywa, tunadhulumiwa, tunaonewa, tunafanyiwa hila,” hadi kuja na kauli za “Tuachwe tupumue,” zinasikika hadi ikulu ya Rais Jakaya Kikwete?

Kelele za upande mmoja wa Muungano zimevuma hadi upande wa pili; ambako sasa wananchi nako wanashinikiza Zanzibar kupewa wanachotaka – serikali yenye mamlaka kamili – lakini papohapo wanadai kuwapo serikali ya Tanganyika.

Hii ni kwa sababu, “bila Tanganyika, hakuna Zanzibar yenye mamlaka kamili.” Bila Tanganyika hakutakuwa na Muungano. Kutakuwa na malalamiko, tuhuma, shutuma na hatimaye Muungano huo utavunjika.

Kabla ya CCM kujitosa katika upinzani wa serikali tatu kwa kusema, “ni kinyume na makubaliano ya mwaka 1964,” kingejipa muda wa kupitia, angalau kidogo, rasimu ya katiba.

Kwa kufanya hivyo kingeweza kugundua hakuna mahali kwenye rasimu iliyotolewa, kunakoonyesha wananchi wanajadili katiba ya mwaka 1964. Kilichoelezwa ni mjadala wa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano, toleo la mwaka 2014.

Hivyo basi, kusingizia muundo wa Muungano wa serikali tatu, ni kinyume na makubaliano ya mwaka 1964; ni kujichosha bure.

Aidha, katiba inayojadiliwa haielekezi kueleza iwapo wananchi wanataka Muungano au hawataki. Haielekezi mjadala wa kuwapo au kutokuwapo kwa Muungano. Rasimu inajadili namna bora ya kuboresha Muungano. Inajadili ambavyo Muungano utadumu.

Ndivyo Rais Jakaya Kikwete alivyoelekeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba; ndivyo alivyoeleza wananchi wakati anazindua tume hiyo, 13 Aprili 2012 na ndivyo hadidu za rejea zinavyoelekeza.

Lakini kuna hili pia: Hata tukikubaliana kuwa Muungano wa mwaka 1964 ulikuwa ni serikali mbili, bado yaliyomo kwenye Muungano wa sasa ni tofuati na yale yaliyokubaliwa wakati huo.

Muungano wa mwaka 1964 ulikuwa na mambo 11. Sasa yameongezeka hadi kufikia 22. Nani ameongeza na kwa ruhusa ya nani? Yameongezwa na Nyerere na Karume? Hapana! Yamepachikwa baada ya Karume kufariki dunia.

Kama Karume angeshiriki katika kuamuru kuongezwa mambo ya Muungano kutoka 11 hadi 22, wala Zanzibar wasingelalamika. Wasingetuhumu kuwapo kwa hila. Wangenyamaza.

Manung’uniko juu ya kuongezwa kwa mambo ya Muungano na upande mmoja wa Muungano unanufaika zaidi kuliko Visiwani, yalianza kuibuka hata kabla Karume hajafariki dunia.

Baraza la Mapinduzi Zanzibar liliwasilisha kwenye vikao vya juu vya Muungano mara kadhaa, maombi ya kutaka kuondolewa kwa baadhi ya mambo kwenye Muungano.

Hassan Nassor Moyo, mmoja wa waasisi wa Muungano amenukuliwa akiliambia Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Aprili mwaka huu, kwamba tokea mwaka 1970, kumekuwapo na kampeni za siri na wazi za kutaka Muungano ufanyiwe marekebisho.

Miongoni mwa mambo ambayo Zanzibar imekuwa ikitaka ni nchi hizi washirika, kila moja kuwa na jeshi lake la polisi; kuwa na mamlaka yake kamili kwenye masuala yanayohusu sarafu, mambo ya nje, uraia, usalama wa taifa na uhusiano wa kimataifa.

Makubaliano haya yaliafikiwa na Nyerere na Karume. Lakini yalishindwa kutekelezwa kwa kile kilichoelezwa na Mwalimu wakati huo, “muda wake haujafika.”

Katika muktadha huo, kupinga mfumo wa serikali mbili kwa madai ya kuenzi wasisi wa Muungano – wakati hata wao tayari waliridhia mabadiliko, ni kujaribu kukwepa ukweli.

Mfumo wa serikali tatu unaopingwa na viongozi wa CCM kwa kisingizio cha gharama, ni nafuu zaidi ukilinganisha na ule wa serikali mbili.

Tofauti na mfumo wa serikali mbili, kwenye muundo wa serikali tatu, kumeainishwa yapi mambo ya Muungano na yapi yasiyokuwa ya Muungano. Umeonyesha idadi ya mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu na wengineo.

Ni tofauti na sasa, ambako mambo ya Tanganyika yamefinyangwa na kuingizwa katika Muungano.

Mfumo wa serikali tatu, utazuia rais wa Muungano kumega nchi vipande kwa kisingizio cha kupeleka maendeleo karibu na wananchi.

Hata hicho kinachoitwa “Zanzibar haitakuwa na fedha za kuchangia uendeshaji mambo ya Muungano,” siyo sahihi. Kwenye mfumo wa Muungano wa serikali tatu, mambo ya Muungano yamebaki machache. Serikali itakuwa ndogo.

Siyo hivyo tu. Viongozi waandamizi Zanzibar, wamekuwa wakisema umasikini wa raia wake unatokana na Muungano. Hivyo wanajua wapi kuna fedha; wapi kuna rasimali; wapi kuna mafuta, gesi na njia zipi watazitumia kuimarisha sekta ya utalii.

Hoja ya CCM kupinga mfumo wa serikali tatu, pengine ingeweza kuungwa mkono iwapo angalau ingeonyesha njia ya kutatua matatizo yaliyopo kwenye Muungano wa serikali mbili.

Wangeonyesha jinsi Tanganyika na Zanzibar zinavyoweza kubaki kwenye Muungano wa serikali mbili, kwa kueleza chombo kitakachosimamia mambo ambayo hayahusiani na Muungano.

Kung’ang’ana na muundo wa serikali mbili, bila kuonyesha njia ya suluhu ya matatizo hayo, ni sawa na kuwalazimisha wananchi waukatae Muungano.

Kwa mfano, kuna mambo mengi ambayo si ya Muungano; lakini yameingizwa kwenye serikali ya Muungano. Mathalani, wizara ya afya, kilimo, ushirika, sheria, utumishi, mifugo, maji na nyinginezo, zinazoweza kuitwa wizara za Muungano, zimepachikwa mambo ambayo hayana uhusiano na Muungano.

Kuna wizara nyingine nyingi zinazoitwa za Muungano, lakini kiuhalisia hazina uhusiano wowote na masuala ya Muungano.

Kwa mfano, wizara ya ulinzi na jeshi la kujenga taifa. Pamoja na kwamba nchi washirika zimeungana kwenye ulinzi, lakini ndani ya wizara hiyo, kuna jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Idara hii siyo ya Muungano. Mbali na kuwa Zanzibar ina jeshi lake linalofanana na hili – Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) – sheria haimlazimishi raia wa Zanzibar kujiunga na jeshi hili.

Vivyo hivyo kwenye wizara ya mambo ya ndani. Ndani ya wizara hiyo, kumeingizwa jeshi la magereza na Zimamoto. Haya si majeshi ya Muungano.

Haijawahi kutokea Kamishina wa Magereza Zanzibar, kupokea maelekezo kutoka anayeitwa, “Kamishina Mkuu wa Magereza nchini” au waziri wa mambo ya ndani.

Hakujawahi kuhamishwa mfungwa (Zanzibar anaitwa “mwanafunzi”) aliyefungwa upande mmoja wa Muungano kupelekwa upande wa pili; au askari wa magereza kutoka upande huu kupelekwa upande ule. Hilo halijatokea na halitatokea kwenye mfumo huu wa sasa wa Muungano.

Ndani ya mfumo wa sheria, hali ni hiyohiyo. Katiba mpya ya Zanzibar toleo la 2010, imeondoa mambo mengi ya sheria kwenye masuala ya Muungano.

Katiba imeng’oa meno hadi Mahakama ya Rufaa ya Jamhuri ambayo ndicho kilionekana chombo cha Muungano. Kifungu cha 99 kimeweka zuio kwa mahakama ya rufaa kusikiliza kesi zozote zinazohusu tafsiri ya katiba; na yale yaliyoanishwa na kutungiwa sheria na Baraza la Wawakilishi.

Yote haya CCM wameyanyamazia. Hawaelezi yatasimamiwa na nani? Kwa utaratibu upi? Nani anaweza kusema hapo kuna Muungano wa serikali mbili? Labda kama ni serikali mbili za kisanii.

Tunawezaje kusema wizara hizi zinashughulikia mambo ya Muungano, wakati yale ambayo hayahusu masuala ya Muungano – Magereza, Sheria, Katiba na JKT hayawezi kusimamiwa na wizara hizo?

Kwa hapa, ambapo wananchi wamefikishwa, wala chama hiki kisijidanganye kuwa kitawafurahisha Zanzibari kwa kuwapa kila wanachokitaka; ili mradi taifa libaki kwenye mfumo wa serikali mbili.

Taifa lililoungana haliwezi kuondoa masuala yanayohusu urai kwenye Muungano, mambo ya nje, uhusiano wa kimataifa au usalama wa taifa; kisha likajiita limeungana kwenye mfumo wa serikali mbili. Haiwezekani.

Haya ni mambo ambayo yanaweza kutekelezeka kupitia mfumo wa serikali tatu. Ukishakubali Zanzibar kuwa na uraia, mambo ya nje, uhusiano wa kimataifa au hata benki yake, upande wa pili wa Muungano utasimamia nini?

Msingi wa serikali ya pili utakuwa upi? Nani anawakilisha taifa hilo lenye muundo wa serikali mbili na kupata uhalali wa kuitwa, “Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?”

Uhuru bandia wa kuipa “Zanzibar mamlaka kamili,” bila kuwapo serikali ya Tanganyika, nao hauwezi kuwa suluhu. Kinachoweza kuitwa, “Zanzibar yenye mamlaka kamili,” kitapatikana kwa kuwapo serikali ya Tanganyika. Si vinginevyo.

Taifa hili tayari limeshuhudia mivutano kwenye nchi nyingine zenye muundo wa muungano kama huu. Tumeshuhudia Muungano wa siku nyingi, kati ya Uingereza na Ireland ya Kaskazini ulivyogubikwa na mitafaruku.

Miongoni mwa yale yanayoleta mitafaruku, ni hoja tata juu ya uhalali wa wabunge wa Bunge la Muungano kutoka Ireland ya Kaskazini kupigia kura bungeni mambo yasiyoihusu Ireland Kaskazini.

Ni sawa tu na hapa kwetu juu ya uhalali wa wabunge kutoka Zanzibar kupigia kura mambo yanayohusu Tanganyika. Huko kutakuwa ni kuelekea kuvunja Muungano. Tayari CCM imetufikisha huko. Huu basi ndio wakati mwafakaa wa kusema, “Hapana!”

error: Content is protected !!