June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bila stika mbaroni Septemba

Spread the love

JESHI la Polisi litaanza mwezi mmoja ujao kukamata madereva wanaoendesha magari yasiyokuwa na viakisi mwanga (Stickers) wakati wa usiku. Anaandika Faki Sosi … (endelea)…

Tamko hilo limetolewa leo na Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani (Trafiki), Naibu Kamishna Mohammed Mpinga alipokuwa katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

DCP Mpinga amesema viakisi mwanga vinatakiwa kutumika kwa magari yote ya abiria na mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 1.5 kwa lengo la kuepusha ajali.

Amesema sharti la kutumia kifaa hicho kinachopaswa kuwekwa pande zote za gari (mbele, nyuma na pembeni mwa gari), limo katika Kanuni iliyotengenezwa kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji wa Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168.

Kifaa hicho kinasaidia kumtambulisha dereva wa gari nyingine iwapo imepata hitilafu na kuwepo kwenye eneo la barabara.

“Ukiweka sticker inakuwa rahisi kwa dereva anayekuja nyuma au mbele yako kuona kuna gari imeharibika barabarani hata kwa umbali wa mita 1,000 kutoka pande zote ilipo gari,” alisema.

Amesema viakisi mwanga vinauzwa na kikosi cha trafiki ambako madereva wanatakiwa kununua huko badala ya kununua maduka mengine ambako huenda kikawa ni feki kisichotoa mwanga inavyotakiwa.

DCP Mpinga ametaja vyanzo vingine vya ajali kuwa ni ubovu wa vyombo vya moto kasoro ambayo kwa mujibu wa utafiti, inachangia ajali kwa asilimia 16; makosa ya kibinaadamu asilimia 76, na mazingira ya barabara asilimia 8.

Katika hatua nyingine, DCP Mpinga ametangaza kwamba kuanzia Jumatatu wiki ijayo, itakuwa ni marufuku kwa madereva kutumia barabara mahsusi kwa mabasi yaendayo kasi.

Barabara ya Kawawa kutokea makutano ya Morocco na Ali Hassan Mwinyi kuunganisha barabara ya Morogoro eneo la Magomeni Mapipa ambayo yenyewe inatokea Kimara Mwisho hadi Kivukoni Feri.

error: Content is protected !!