August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bil 7 zateketea 21st Century

Spread the love

KIWANDA cha 21st Century kilichopo eneo la Kihonda mjini Morogoro kimepata hasara ya zaidi ya Sh. 7 Bil katika Idara ya Useketaji (Weaving) pekee, anaandika Christina Haule.

Akizungumza mbele ya uongozi wa Chama Cha Wafanyakazi wa Viwanda, Taasisi za Fedha Huduma na Ushauri (TUICO), Florence Mbaga ambaye ni Meneja Utawala na Rasilimali Watu wa 21st Century amesema kuwa, kiwanda hicho kimepata hasara kubwa ambayo mpaka sasa jumla ya hasara hiyo bado haijafahamika kutokana na kuteketeza kwenye maeneo matatu muhimu.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na nguo zilizozalishwa na vitambaa ambavyo vilinunuliwa na kuandaliwa kwa ajili ya kuzalisha nguo, majengo pamoja na mitambo au mashine za kuzalisha nguo hizo. Kiwanda hicho kiliungua tarehe 19 Julai mwaka huu.

Mbaga amesema, kiwanda hicho kinaendelea kufanya tathmini ili kujua hasara kamili kwa kila eneo licha ya kuwa mpaka sasa wamebaini hasara hiyo katika eneo moja la nguo na vitambaa.

Amesema kuwa, katika kuhakikisha wanawajali wafanyakazi wao, wameweza kuwapatia kifuta jasho wale walioshirikiana nao kwa siku nzima katika kuzima moto huo na sasa wanaendelea na juhudi za kukarabati idara ya useketaji ili waweze kurejesha wafanyakazi wote kwa pamoja ndani ya mwezi mmoja hadi miwili.

Amesema kuwa, mpaka sasa wafanyakazi 50 kati ya 600 wa idara ya useketaji wamepewa likizo ya mwezi mmoja na kwamba, watarejeshwa kazini kwa awamu huku wafanyakazi wengine wakibaki kiwandani kwa ajili ya kufanya usafi katika eneo lililoungua na wengine wakiendesha baadhi ya mashine zilizokwishatengenezwa.

Paul Sangeze, Mwenyekiti wa TUICO Taifa amepongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kukubali na kufunga nao mkataba wa kuwapa likizo, mshahara wa mwezi mmoja pamoja na posho ya 80,000 kila mfanyakazi wa idara iliyoungua licha ya kupata janga hilo.

Akizungumzia masuala ya usalama mahali pa kazi Jones Majura, Mkuu wa Sekta ya Viwanda (TUICO) ametoa wito kwa viwanda vya chuma na mabati kuhakikisha wanazingatia sheria ya afya na usalama kazini kwa kuwa wengi wao hawajali.

error: Content is protected !!