SERIKALI ya Tanzania, imepanga kutumia Sh. 40 bilioni, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji, kwenye mashamba ya uzalishaji wa mbegu ya Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA). Anaripoti Nasra Bakari, DMC … (endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatatu, tarehe 31 Mei 2021, na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, akimjibu Mbunge Viti Maalum asiye na chama bungeni, Nusrat Hanje.
Katika swali lake, Hanje alihoji mpango wa Serikali katika kutumia mashamba ya uzalishaji mbegu bora, hasa zao la alizeti ili kuinua uchumi wa wananchi wa singida, wanaotegemea kilimo cha zao hilo.
Baada ya Hanje kuhoji hayo, Bashe amesema Serikali imeendelea kuweka mikakati ya kuongeza upatikanaji wa mbegu bora za mafuta nchini, kwa kutenga fedha Sh. 40 bilioni, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba ASA.
“ili kuzalisha mbegu za alizeti na mbegu za mazao mengine kama vile mahindi, mpunga, michikichi, pamba, Ngano, ufuta na mazao ya bustani. Lengo ni kuondokana na utaratibu wa mkulima na wazalishaji mbegu, kwenda shamabani kwa pamoja,” amesema Bashe.
Naibu Waziri huyo wa Kilimo amesema, miundombinu hiyo ikikamilika, uzalishaji mbegu za alizeti nchini, utaongezeka kutoka tani 538.71 msimu wa 2019/20, hadi kufikia tani 10,000 (2019/30).
Bashe amesema, mbegu hizo zitatosha kutumika katika eneo la hekta 1,250,000, zinazoweza kuzalisha tani 500,000 za mafuta ya kula nchini.
“Aidha, katika kipindi cha miaka mitatu uzalishaji wa mbegu wa ASA umeendelea kuongezeka, kutoka tani 74.2 (2016/17) hadi kufikia tani 166.0 (2019/20) na sekta binafsi ilizalisha tani 372.71,” amesema Bashe.
Leave a comment