January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bil 3.91 kusambaza umeme vijiji 13 Meatu

Mafundi umeme wakiwa kazini

Spread the love

SERIKALI imesema, kiasi cha Sh. 3.91 bilioni zinatarajia kutumika kwa ajili ya kupeleka umeme kwenye vijiji 13 vilivyopo katika Jimbo la Meatu. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Vijiji vitakavyonufaika na mradi huo ni Mwenge, Sungamwabuya, Kabondo, Bulyashi Center, Zahanati ya Bulyashi, Mwamishali Sekondari, Mwambiti, Mwanyahina, Bulyanaga, Mwambegwa, Kimali Sekondari na Nkoma.

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage alipokuwa akijibu swali la Mbuge wa Meatu, Meshack Opulukwa (Chadema).

Opulukwa alitaka kujua, lini umeme utawashwa katika Kata za Mwanjolo, Bukundi, Mwamalola, Imalaseko, Mwamanongo na Mwabuzo vilivyopo katika Jimbo la Meatu.

Mwijage amesema, mradi huo utagharimu Sh. Bilioni 3.91 na kwamba, kazi za mradi huo zitahusisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 33 urefu wa kilomita 76.4, ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 0.4 urefu wa kilomita 28.6, ufungaji wa transfoma 11.

Mradi wa kusambaza umeme Meatu amesema, unatekelezwa na Mkandarasi LTL Projects Ltd na kuwa, kuchelewa kukamilika kwa mradi huo kumesababishwa na kuchelewa upatikanaji wa vifaa vya usambazaji hasa vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi pamoja na nguzo.

Amesema, mradi huo unatarajia kukamilika mwishoni mwa Agosti, 2015.

Kuhusu kuwasha umeme kwenye Kata za Mwanjolo, Bukundi, Mwamalola, Imalaseko, Mwamanongo na Mwabuzo amesema, kata hizo hazikuingizwa katika utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini awamu ya pili kutokana na ufinyu wa bajeti.

error: Content is protected !!