March 5, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Bil 2 zatengwa kukuza Kilimo Biashara

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Binafsi ya kusaidia sekta ya kilimo nchini (PASS) Bw,Nicomed Bohay

Spread the love

TAASISI binafsi ya kusaidia Sekta ya kilimo Tanzania (PASS) imetenga kiasi cha Sh. 2 bilionikwa ajili ya kuwawezesha Wahitimu 100 kila mwaka kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Vijana wengine waliohitimu ili kuweza kuanzisha miradi ya Kilimo Biashara kwa kutumia taaluma yao. Anaripoti Christina Haule, Morogoro … (endelea).

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya PASS, Nicomed Bohay amesema hayo jana baada ya kuingia makubaliano na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) yenye lengo la kuwaandaa kwa vitendo Wajasiliamali vijana wahitimu wa fani mbalimbali hususani katika sekta ya Kilimo.

Boyah amesema kuwa upatikanaji wa fedha hizo umelenga kuanzishwa kwa miradi 100 ya majaribio katika chuo hicho kupitia mpango maalum wa utoaji wa mazoezi na majaribio kupitia vituo maalum (Incubators) vyenye lengo la kutoa uzoefu kwa wajasiliamali vijana.

“Baada ya kuona uwepo wa changamoto ya wahitimu katika masuala ya kilimo pamoja na fani nyinginezo wakishindwa kushiriki katika shughuli za kilimo-biashara baada ya kukosa mitaji PASS kupitia Idara yake ya Agribusiness Innovation Center (AIC) imeona ije na mpango huu,” amesema Boyah.

Amesema mpango huo utawawezesha wajasiliamali vijana kupata mitaji pamoja na nyenzo mbalimbali katika maeneo maalum kwa lengo la kuwaandaa kuwa Wajasilimali watakao weza kumiliki Miradi ya Kilimo-Biashara.

Bohay amesema, kipaumbele kitatolewa kwa wajasiliamali vijana watakaojihusisha na uzalishaji wa mbogamboga kwenye mahema (green house), ufugaji wa kisasa wa samaki, kuku, mbuzi, usindikaji na viwanda vidogo vya kuzalisha bidhaa zinazotokana na kilimo kwa ajili ya masoko ya ndani na nje ya nchi.

“Wenzetu wa Chuo Kikuu Cha Sokoine (SUA) wametoa eneo la kutoshereza kwa miradi ya wajasiliamali vijana kwa lengo la kuhakikisha vijana wetu wanapata mahali pa kuanzia kabla ya kujitegemea,” amesema Bohay.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUA, Prof. Raphael Chibunda amesema kuwa ushirikiano huo na Taasisi ya kusaidia sekta binafsi ya kilimo PASS umekuja wakati muafaka na kuwataka wahitimu pamoja na watafiti chuoni hapo kuchangamkia fursa hiyo.

“Kwetu sisi mradi huu wa kuwalea wahitimu wetu kwa kuwapatia mitaji, nyenzo na ushauri na maeneo maalumu ya kutekeleza kile walichokisoma darasani kwa vitendo ni faraja sana kwani siku zote tumekuwa tukiwaandaa vijana wetu waweze kukabiliana na changamoto za Maisha huko mtaani kwa kutumia elimu waliyoipa hapa chuoni,” amesema Prof. Chibunda.

“Sasa tunawapa fursa hiyo hapa hapa chuoni kabla hawajaingia huko mtaani, wataondoka hapa wakiwa ni wajasiliamali mahili wa kilimo biashara na mchango wao kiuchumi kwa taifa na jamii utaongezeka sana,” amesema Prof. Chibunda.

Mpango huu unatajwa kuwa suluhu ya changamoto ya ajira kwa wahitimu hususani wa masuala ya kilimo ambapo kupitia SUGECO Vijana watatambuliwa na kupitia katika vituo maalumu vya uwezeshaji (Incubators) ambapo baadae watakuwa na uwezo wa kujiajiri na kujiendeleza kiuchumi.

error: Content is protected !!