MWANAHARAKATI huru, Bihimba Mpaya, amechangia ujenzi wa msikiti katika Madrasa ya Muhajirina, iliyoko Mtaa wa Kigezi Chini, wilayani Ilala, Jiji la Dar es Salaam, kwa kutoa matofali 1,750 pamoja na mifuko 10 ya saruji. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Msada huo umekabidhiwa leo tarehe 17 Novemba 2023 na Bihimba kwa kiongozi wa madrasa hiyo, Ostadh Amir Mussa Mohammed, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Bihimba, aliwataka waislamu wengine wajitokeze kuchangia ujenzi wa msikiti ili kuwezesha kazi ya uenezaji dini kwa waumini wengine.
“Nimetoa misaada mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa madrasa na msikiti ili kuhakikisha kazi ya Allah ya kueneza usilamu kwa waumini wake inafanyika. Waislamu wenzangu hamjachelewa toeni michango sababu msikiti lazima ujengwe,” amesema Bihimba.
Katika hatua nyingine, Bihimba amesema anawasiliana na wadau wengine, ili kuona namna ya kujenga kisima katika madrasa hiyo, kwa ajili ya upatikanaji maji.
Mwanaharakati huyo ametoa msaada huo baada ya Ostadh Mohamed kuwaomba wasilamu wachangia ujenzi wa madrasa na msikiti, ili kuondoa changamoto ya waumini kusoma pamoja na kuswali nje ya mti.
“Tunashukuru kwa msaada alioutoa Bihimba, lakini tunaomba wanaotusikiliza sasa hivi wajue bado tunahitaji msaada na madrasa yetu bado tuna ujenzi. Tulikuwa tunasoma kwenye nyumba ya makuti lakini kutokana na mvua imeharibika hivyo tunasoma kwa shida chini ya mti na mvua hii,” amesema Sheikh Mohamed.
Leave a comment