Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa BIBI TITI MOHAMMED; Mwanamke wa nguvu aliyedaiwa kutaka kumpindua Nyerere
Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

BIBI TITI MOHAMMED; Mwanamke wa nguvu aliyedaiwa kutaka kumpindua Nyerere

Spread the love

 

MIAKA ya hivi karibuni kumeibuka mtindo wa wanawake kujiita au hata kuitwa ‘mwanamke wa nguvu’ lakini wengi wamemsahau Bibi Titi Mohammed, ambaye alikuwa hasa ‘mwanamke wa nguvu’ wakati wa mapambano ya kuikomboa Tanzania yetu.

Leo nimeona si vibaya kuwakumbusha juu ya mwanamke aliyepata kujitoa kwa moyo wote ili nchi yetu ya Tanzania iwe huru lakini inaelezwa kuwa maisha yake ya mwisho hapa duniani yalijawa na huzuni na upweke sana.

Bila shaka vijana wengi wa kizazi hiki hawamjui kabisa mama huyu shupavu na wamekuwa wakisikia au kuiona tu barabara ya Bibi Titi.

Kati ya miaka ya 1970 mwanamke mwenye wajihi wa ushupavu Bibi Titi Mohammed alihusishwa katika tukio la kujaribu kutaka kuipindua serikali ya wakati huo iliyokuwa chini ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Bibi Titi alihukumiwa kifungo cha maisha jela. Haikuwa rahisi kwake kulipokea hilo, ingawa baadae alitolewa lakini ameendelea kukana kabisa kuhusika na tukio hilo mpaka umauti ulipomfika mwaka 2000.

Kihistoria, Bibi Titi Mohammed aliingia TANU kwa kushawishiwa Schneider Plantan aliyekuwa mmoja wa viongozi wa chama cha TAA ambacho baadaye kiliitwa TANU. Schneider alikuwa rafiki yake Boi Selemani aliyekuwa mumewe Bibi Titi. Wanahistoria wengi huandika Nyerere kwamba ndiye alimuingiza Bibi Titi kwenye chama wakati si kweli.

Bibi Titi Mohammed

Baada ya kuingia TANU alipata kadi namba 16 na mumewe alipewa kadi 15. Bibi Titi alikuwa mwasisi wa Umoja wa Wanawake Tanganyika (UWT) uliokuja kuundwa rasmi mwaka 1962.

Wakati wa harakati za kupigania uhuru alisimamia vikundi vya muziki kama vile ‘lelemama’ na mara zote alitangulia kuzungumza na umati mkubwa kabla hata Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere hajahutubia Watanganyika katika mikutano yake.

Alikuwa na maneno makali dhidi ya ukoloni na alikuwa ana nguvu kubwa ya ushawishi. Akiwa na miaka 26 tu alikuwa ni mmoja kati ya wanawake wachache walioaminiwa katika kuongoza mapambano dhidi ya udhalimu waliokuwa wakifanyiwa Watanganyika.

Mwaka 1955, Nyerere na Bibi Titi Mohammed walifanya mkutano mkubwa huko Tabora.

Hii ni kutokana na mwaliko walioupata kutoka kwa watu wa huko. Ikumbukwe kuwa Tabora ya wakati huo ilikuwa na hamasa kubwa katika kudai uhuru.

Hivyo mualiko ulitoka kwenye kamati ya wazee kama Hassan Mohamed Ikunji, Hamis Khalfan, Swedi Mambosasa, Germano Pacha, Juma Mrisho, Shaaban Mohamed Silabu, Bilali Rehani Waikela na  Mohamed Mataka.

Kuna mikutano mingi tu ya harakati za uhuru aliyoongoza Bibi Titi mfano ule wa Mombasa akishirikiana na Tom Mboya katika Ukumbi wa Tononoka.

Kiujumla mkutano mkuu wa kwanza Tabora ulifungua njia kukubalika kwa TANU baadaye kulifanyika ‘Azimio La Tabora’. Azimio hilo liliongozwa na Nyerere na wengine kama Sheikh Suleiman Takadir, Mzee Jumbe Tambaza, Juma Selemani na Bibi Titi.

Bibi Titi Mohammed

Hivyo, alikuwa mmoja ya waasisi wa ‘Azimio La Tabora’. Baada ya uhuru 1961 alichaguliwa kuwa mbunge na waziri pia. Halikuwa jambo la kushtua kwani alistahili.

Mwaka 1963 inaelezwa kulitokea kutokuelewana kati ya Bibi Titi na Mwalimu Nyerere wakati wa  mkutano wa Halmashauri Kuu ya TANU uliofanyika Ukumbi wa Karimjee.

Hapo walitupiana maneno makali kabisa. Inaelezwa kuwa kati ya mambo mengine mengi sababu zilikuwa ni Halmashauri Kuu ya TANU kulivunja Baraza la Wazee wa TANU ambao kwa hakika walisaidia wakati wa harakati za uhuru. Hilo lilipingwa na Bibi Titi.

Jambo lingine linaelezwa na mwandishi Said Mohammed katika maandishi yake kuwa ni uamuzi wa Bibi Titi kuitetea Jumuiya ya Waislamu ya Afrika Mashariki (East African Muslim Welfare Society (EAMWS) ambapo Mwalimu Nyerere alipinga hilo kwani aliona ni hatari kuchanganya ‘Dini na Siasa’.

Bado kumekuwa na ugumu kupata taarifa hasa chanzo cha mtifuano huo kwani wengi wanaelezea mkutano huo ulikuwa tu ni nafasi ya kuonesha tofauti zao waziwazi.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1965 Bibi Titi na Tewa (Tewa Said Tewa alikuwa rais wa jumuiya ya EAMWS) wakapoteza viti vyao ndani ya TANU na serikalini pia.

Mwaka 1968, Bibi Titi alikamatwa na kuhusishwa na tukio la ‘uhaini’. Mahakama ilimkuta na hatia.

Hivyo, alihukumiwa kwenda jela maisha. Mwaka 1972 aliachiwa huru kwa msamaha wa rais. Bado aliendelea kukana kuhusika kabisa na tukio hilo.

Alirudi na kuendelea na maisha yake ya kawaida huko maeneo ya Temeke. Inaelezwa kuwa alipoteza kumbukumbu nyingi za harakati za uhuru kama vile picha na taarifa nyingi za vikao na mkutano ya TANU. Baadaye alihamia Upanga.

Aliporudi uraiani walikuwa na urafiki na Mwalimu Nyerere kama zamani (Kuna uwezekano hakukuwa na ugomvi mkubwa kati yao kama ilivyotiwa ‘chumvi’).

Aliumwa na kupelekwa na serikali ya Tanzania katika hospitali ya Net Care huko Afrika ya Kusini. Alifariki dunia akiwa hapo hospitalini akipata matibabu tarehe 5 Novemba 2000 (Mwaka mmoja baada ya kifo cha Baba wa Taifa).

Hakika ni ‘Mama wa nguvu’ na haitoshi tu ni ‘MWANAMKE WA NGUVU’  katika historia ya Tanzania.

Makala hii imeandaliwa na Francis Daudi

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!