WANAUME wameshauriwa kuacha kununua wanawake Makahaba ili kuua biashara hiyo haramu katika maeneo mbalimbali hapa nchini, anandika Dany Tibason.
Imeelezwa bungeni kuwa kama kila mwanaume ataacha kununua ngono, biashara hiyo itakwisha yenyewe kwa kuwa wanawake wanaouza miili yao hawatakuwa na soko.
Hayo yameelezwa leo bungeni na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk.Khamisi Kigwangala alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Geita Vijijini, John Kanyasu(CCM).
Mbunge huyo alihoji, agizo la Dk. Kigwangala la kuwakamata wanawake wanaojiuza.
“Je zoezi hilo limefanikiwa kwa kiasi gani nchi nzima”aliuliza Kanyasu.
Akijibu swali hilo, Dk.Kigwangala, aliwaasa wanaume nchini kuacha kujihusisha na biashara hiyo yenye madhara kwa familia zao kiuchumi na kijamii kwani wakiwaacha wanawake hao watakosa soko.
“Kwa Mwanaume kuwa mteja wa biashara hiyo nalo ni kosa kisheria,”amesema Dk Kigwangallah.
Pia Naibu Waziri huyo alikiri kuwa kumekuwa na ongezeko na vitendo vya wanawake kujiuza katika maeneo mbalimbali hasa katika maeneo ya Miji mikubwa kama vile Dar es salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya na Dodoma.
Dk Kigwangallah alisema kwa mujibu wa vifungu vya sheria namba 176(a),176A vya sheria ya makosa ya jinai kitendo cha mwanamke kuishi akitegemea kipato chake au sehemu ya kipato chake kutokana na ukahaba ni kosa kisheria.
“Hivyo katika kuhakikisha kuwa sheria hii inatekelezwa viongozi katika mikoa mbalimbali ukiwemo Dar es salaam wamekuwa wakiwakamata na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria wanawake wanaojiuza.
Amesema serikali kupitia Jeshi la Polisi inaendelea kufanya ‘Operation’ ya kubaini na kuwakamata wamiliki wenye madanguro yanayotumiwa na makahaba hao.
“Nitumie fursa hii kuwataka wanawake wanaofanya biashara hii kuacha mara moja na kutafuta shughuli nyingine ya kujipatia kipato cha halali,”amesema
Katika swali la nyongeza Mbunge wa Mlimba, Susaz Kiwanga(Chadema) alitaka kujua serikali inawachukulia hatua gani watu wanaofanya mapenzi ya jinsia moja.
Akijibu, Dk Kigwangala amesema sheria inakataza watu wa jinsia moja kufanya mapenzi hata mwanaume kufanya mambo ya kike pamoja na mwanmke kufanya mambo ya kiume.
Leave a comment