January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Benki za Tanzania zaahidi kuongeza ukopeshaji

Spread the love

 

LICHA ya janga la corona kuathirika ukopeshaji, Benki nchini Tanzania, zimeahidi kuongeza mikopo kwa ajili ya sekta binafsi kufuatia kuimarika kwa uchumi wa dunia na hatua zinazochukuliwa na serikali kuweka sawa huduma hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Taasisi hizo za fedha ziliweka bayana mpango huo Ijumaa ya tarehe 26 Novemba 2021, jijini Dodoma kwenye Mkutano wa 20 wa Taasisi za Fedha (COFI 2021), nakusema, kuimarisha ukopeshaji kutasaidia uzalishaji na kuukwamua uchumi wa taifa kufuatia janga hilo, linaloitikisa dunia.

Kwa mujibu wa viongozi waandamizi wa benki hizo, hilo litawezekana kwa sababu benki nchini zina uwezo kifedha kukopesha zaidi na tena kwa riba rafiki.

Ili yote hayo yaweze kufanyika kwa ufanisi, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, alisema juhudi za pamoja ni muhimu na ushirikiano wa wadau wote unahitajika.

“Janga la Uviko-19 limekuwa na athari kubwa kwenye benki zetu kuikopesha sekta binafsi,” alisema Ruth alisema hayo wakati anawasilisha maada kuhusu kuongeza mikopo kwa sekta binafsi baada ya janga la Uviko-19.

Wasilisho lake lilikijita kwenye wajibu wa serikali, taasisi za fedha na sekta binafsi katika kuongeza upatikanaji wa mikopo na mchango wa wadau hao kufufua ukuaji wa uchumi.

“Ili kuchochea ukopeshwaji wa sekta binafsi baada ya janga la Uviko-19, mambo kadhaa yanabidi kufanywa na wadau husika. Hatua hizi zinahitaji mbinu shirikishi ili kuhakikisha matokeo endelevu ya kiuchumi,” alisema Ruth

Aidha, alisema tayari kuna mazingira wezeshi ya kuongeza mikopo na ustahimilivu stahiki wa kisekta wa kuchochea kufufua ukopeshaji.

Hii ni pamoja na kuendelea kuimarika kwa uchumi wa dunia ambao baada ya kupigika na uviko hadi kudorora kwa asilimia 3.1 mwaka 2020 sasa Shirika la Fedha Dunia (IMF) linasema utakua kwa asilimia 5.9 mwaka huu.

Kuimarika huko kutasababisha uchumi wa Tanzania nao pia kufanya vizuri ukikua kwa asilimia tano mwaka huu ukilinganisha na ukuaji wa 2020 wa asilimia 4.8.

Kwa upande wake, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof Florens Luoga alisema hali itakuwa nzuri zaidi 2022 kutokana na kupungua kwa athari za Uviko-19 kutakasababisha uchumi wa taifa kukua kwa asilimi 5.2 mwaka kesho.

Mkutano wa 20 wa Taasisi za Fedha uliofunguliwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan uliandaliwa na BoT kwa kushirikiania na Umoja wa Mabenki nchini (TBA) ili kujadili uimarishaji wa uchumi wa Tanzania kufuatia janga la Uviko-19.

Katika mada yake, Ruth alisema sababu nyingine ya kuwepo mazingira sahihi ya kufufua ukopeshaji ni kutokana na sera sahihi za serikali ambazo pamoja na kutoa kinga madhubuti dhidi ya Uviko-19 pia zimesaidia sekta ya benki kustahimili vishindo vya janga hilo.

Ustahimilivu huo ulipelekea rasimali fedha za benki nchini kuongezeka kwa asilimia 4.16 mwaka 2020 hadi Sh.34.68 trilioni huku amana nazo zikiongezeka karibu kwa asilimia nne hadi Sh.24.77 trilioni.

Alisema, mitaji nayo ilendelea kuwa sawa mwaka jana na karibu benki zote zilipata faida zikiongozwa na NMB iliyopata faida kubwa kuwahi kutengenezwa na benki yoyote nchini ya Sh.206 bilioni.

“Hali hii ilizifanya benki kuendelea kulihudumia taifa kipindi chote za janga la Uviko-19 bila kuathiri wateja na wafanyakazi wake,” alisema Ruth na kuongeza, taasisi hizo pia zilichangia juhudi za taifa za kukabiliana na Uviko kwa kuchangia zaidi ya Sh.1 bilioni.

Hatua nyingine za kisera zilizochukuliwa na BoT mwaka 2020, ni pamoja na kupunguza riba za hati fungani za serikali na kupunguza hadi asilimia sita kiwango cha sehemu ya amana za benki kinachotakiwa kuwekwa benki kuu (SMR).

Pia, BoT ilishusha riba ya mikopo kwa benki (discount rate) hadi asilimia tano kuzipunguzia gharama za kukopa na kuziongezea ukwasi. Hatua nyingize za kisera zilichukuliwa Julai 2021 ili kuongeza msukomo wa kasi ya kuikopesha sekta banafsi na kuharakisha ufufuaji wa uchumi.

Hatua hizo ni pamoja na kulegeza masharti ya usajili wa mawakala wa benki, ukomo wa riba kwenye akaunti za makampuni ya watoa huduma za
fedha kwa njia ya simu za mkononi na kuanzishwa kwa mfuko maalum wa kuzikopesha benki na taasisi za fedha wenye thamani ya Sh.1 trilioni.

“Hatua hizi zilizochukuliwa na BoT Julai 2021 na kuimarika kwa uchumi wa dunia kumesababisha kuongezeka kwa kiasi kikubwa ukopeshaji wa sekta binafsi,” alisema Ruth

Kabla ya Uviko-19 mikopo kwa ajili ya sekta binafsi ilikuwa inakua vizuri na kifikia asilimia 11.1 mwishoni mwa mwaka 2019 lakini hali ilibalika ghafla baada ya dunia kugubukwa na janga hilo.

Ukuaji huo ulipungua hadi asilimia 5.5 katikati ya mwaka jana na hali ilizidi kuwa mbaya miezi iliyofuata. Ruth alisema kumekuwepo na maendeleo mazuri hivi karibuni kutokana na kendelea kuimarika kwa uchumi wa dunia na jitihada za serikali pamoja na benki kuimarisha na kurahisisha upatikanji wa mikopo.

error: Content is protected !!