July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Benki ya UBA yamwaga vitabu 1,500 Kigamboni

Spread the love

BENKI ya UBA Tanzania kupitia taasisi ya UBA Foundation chini ya mpango wa ‘Read Africa Initiative’ imetoa vitabu 1,500 vya fasihi kwenye shule za serikali zilizopo wilaya ya Kigamboni, Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Benki hiyo imetoa msaada huo iliotembelea Shule za Sekondari za Nguva Sekondari, Aboud Jumbe sekondari na Pembamnazi sekondari zote zipo wilayani Kigamboni.

Vitabu hivyo vilikabidhiwa kwa Sara Msafiri , Mkuu wa wilaya ya Kigamboni leo tarehe  11, Julai 2019 na uongozi wa UBA Benki ukiongozwa na Geofrey Mtawa , Mkuu wa Kitengo cha Biashara Ndogondogo na za kati, Mkuu wa kitengo cha Dijitali,  Asupya Nalingigwa na Afisa Mawasiliano, Anitha Pallangyo na Msimamizi wa Tovuti ya Benki, Kassim Riyami.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, Msafiri ameipongeza benki ya UBA Tanzania kwa mchango mkubwa inayotoa kwenye sekta ya elimu, ikiwemo kutoa vitabu kwa shule za sekondari zenye uhitaji wa vitabu zilizopo wilayani humo.

“Vitabu hivi vilivyotolewa na benki ya UBA Tanzania, vitasaidia katika kuwajengea vijana wetu kupenda kujisomea na kujiwekea utaratibu wa kujisomea mara kwa mara, pamoja na kuwaongezea uwezo katika masomo yao,” amesema Msafiri wakati wa ziara hiyo.

Msafiri ameeleza kuwa, vitabu hivyo vitasaidia kuongeza idadi ya vitabu vyenye ubora kwenye maktaba za shule husika.

Geofrey amesema vitabu hivyo ni vya hadhi ya juu Afrika, ambavyo vimeboreshwa zaidi ili kuwawezesha wanafunzi na walimu kuvielewa kwa lugha rahisi na yenye kuelimisha.

Mbali na kutoa vitabu hivyo, UBA Tanzania imekua ikisaidia sekta ya elimu kwa kutoa vitabu kwenye shule mbalimbali ikiwa ni pamoja na wilaya za Ilala, Temeke, Kisarawe Na Pwani, pamoja na kutoa elimu ya ujasiriamali bure kwa vijana na wanawake kupitia mpango wao wa ‘Each one teach one’.

Baadhi ya vitabu vilivyotolewa na benki hiyo ni vile vinavyotumika kwenye mitaala ya Tanzania kama Things Fall Apart, The Girl That Can, The Fisherman, na vinginevyo vingi kutoka kwa waandishi mashuhuri kutoka Nigeria na hutumika kwenye mitaala ya shule mbalimbali Africa.

Mtawa  amesema UBA inafurahi kuongoza usukani kwenye kuwajengea vijana hususani wa shule za sekondari tabia ya kujisomea, kupitia mpango wake wa Read Africa Initiative.

Amesisitiza kuwa, elimu ni miongoni mwa maeneo makuu matatu ambayo benki ya UBA imejikita kusaidia katika Afrika. Kama moja ya njia ya kurudisha kwa jamii ambao ni wadau wakubwa wa benki, maeneo mengine yakiwa ni afya na mazingira.

UBA Tanzania ambayo makao makuu yake yapo barabara ya Nyerere jirani na daraja la Mfugale (Tazara Flyover), ni kampuni tanzu ya UBA Group moja kati ya benki zinazoongoza duniani, iliyopo kwenye nchi Zaidi ya 20 Africa na kwenye vituo vikubwa vya biashara New York, Paris na London uingereza.

Inatoa huduma za kawaida za kibenki, pamoja na za kidijitali na imetunukiwa tuzo ya kuwa benki bora na inayoongoza kidijitali Afrika kwa mwaka 2018 ambazo hutolewa na Euromoney.

error: Content is protected !!