Sunday , 19 May 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Benki ya Kilimo: Ni mkopeshaji au dalali?
Makala & Uchambuzi

Benki ya Kilimo: Ni mkopeshaji au dalali?

Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Tanzania
Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Kassim Majaliwa, amewasilisha bajeti ya wizara yake, bungeni mjini Dodoma na kumwagia sifa Benki ya Kilimo. Amesema, benki hiyo ndio mkombozi wa taifa. Anaandika Saed Kubenea, Dar es Salaam … (endelea).

Benki hiyo, kwa mujibu wa waziri mkuu, imenufaisha maelfu ya wakulima, wavuvi na wafugaji, Bara na Visiwani. Ametaja jumla ya watu walionufaika na mikopo iliyotolewa na benki, kuwa ni 1,522,751.

Pamoja na ukweli kuwa kuanzishwa kwa benki hii, kulilenga kuwapo uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya kilimo na viwanda, pamoja na kuongeza thamani bidhaa za kilimo, lakini hali ni tofauti na hicho kilichokusudiwa.

Kwamba, kinachoendelea katika benki hiyo, kinatofautiana kwa kiwango kikubwa na kile kilichoelezwa na waziri mkuu bungeni. Ni tofauti na kinachopigiwa chapuo na mawaziri kadhaa waliopita wa wizara ya kilimo na watendaji wengine wa serikali.

Benki ya maendeleo ya Kilimo, siyo mkombozi wa wananchi. Siyo mkombozi wa wakulima, wavuvi wala wafungaji. Kipaumbele kikubwa cha beki hii, ni kunufaisha watendaji wake. Sababu kubwa ni mbili:

Kwanza, Benki ya Kilimo ilianzishwa mwaka 2009, ikiwa ni dirisha ndani ya Benki ya Rasilimali – Tanzania Investment Bank (TIB). Benki hii ilikuwa na shughuli ya pili kwa umuhimu, baada ya shughuli ya kwanza ya “kuongeza bajeti ya serikali kwa ajili ya mradi wa Kilimo Kwanza.”

Ilitarajiwa kuanzishwa ikiwa na mtaji wa dola za Marekani 500 milioni (sawa kwa wakati huo, Sh. 800 bilioni) au Sh. 1.2 trilioni kwa sasa.

Fedha hizo zingepatikana iwapo serikali ingetenga kiasi cha bilioni 100 kila mwaka. Lengo likiwa ni kukopesha wakulima wadogo wadogo kwa masharti na riba nafuu! Benki hii muhimu iliishia kuambulia Sh. 60 bilioni hadi Aprili 2015.

Benki ya Maendeleo ya Kilimo ilianza rasmi kuwa taasisi ya kibenki inayojitegemea, Septemba mwaka 2011.

Kazi kuu ya Benki ikiwa ni uhamasishaji utoaji wa huduma za kifedha na huduma zisizo za kifedha kwa sekta ya kilimo, ikiwamo kutoa vifaa vya muda mfupi, kati na mrefu kwenye sekta ya kilimo.

Nyingine, ni kuchochea utoaji wa mikopo kwa sekta ya kilimo, hivyo kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta hiyo; kuwa Benki Kuu inayofadhili sekta ya kilimo, yenye mikakati ya kujenga uwezo na mipango ya kuimarisha mnyororo wa thamani kwa sekta kilimo.

Aidha, benki ilikuwa na jukumu la kufadhili shughuli za kilimo, uvuvi, ufugaji nyuki na mifugo. Kuimarisha mnyororo wa thamani kwa njia ya mafunzo, utafiti na ushauri.

Pamoja na serikali kutoa mtaji wa Sh. 60 bilioni – Septemba 2014 – ili kuendesha shughuli za benki hiyo, lakini taarifa za ukaguzi zinaonesha tofauti.

Badala ya kutoa mikopo kwa sekta ya kilimo ambayo ndiyo shughuli yake kuu, menejementi ya Benki imekuwa ikiwekeza sehemu kubwa ya fedha zake katika amana za kudumu.

Kufikia 31 Desemba 2016, jumla ya Sh. 54.70 bilioni, zilikuwa zimewekezwa kwenye amana za kudumu, ambayo ni karibu asilimia 91 ya mtaji.

Kama hiyo haitoshi, kati ya Sh. 3.95 bilioni ya mikopo iliyotolewa, Sh. 1.71 bilioni, ni mikopo iliyotolewa kwa watumishi na Sh. 2.23 bilioni 2.23 tu ndio zimekuwa mkopo kwenye sekta ya kilimo.

Hata katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2019/20, ukurasa 57 kunaonesha benki ilitoa mikopo kwa wakulima 1,049,370 wa mahindi, mpunga, shayiri, kahawa, korosho, karafuu, miwa, mbogamboga, ufugaji wa samaki na wengineo, wenye thamani ya Sh. 95.1 bilioni tu.

Hapa ni kipindi kile ambacho taifa lilikuwa linaimbiwa tunataka kujenga Tanzania ya Viwanda, lakini hatuoni ni kwa jinsi gani benki hiyo iliwekeza kwenye ujenzi huo.

Pili, ukirejea nyaraka za serikali yenyewe, kama vile hotuba ya waziri wa kilimo kwa mwaka wa fedha 2017/18, alieleza benki hiyo, itaboresha huduma za kibenki kwa kuanzisha mazao maalum kwa wakulima wadogowadogo, kulingana na mnyororo husika wa thamani na vipaumbele vya mikoa husika.

Kwamba, benki imepanga kufanya maandalizi ya kutoa mikopo ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji, katika maeneo yaliyoainishwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.

Vilevile, benki imepanga kuwajengea uwezo wakulima wadogowadogo, wafanyakazi wa benki yenyewe; benki nyingine na wadau mbalimbali wa kilimo.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe

Mbali na kwamba vipaumbele hivyo vya mikoa havijulikani uhusiano wake na “malengo mapana ya taifa,” ili kuelekeza mikopo hiyo kwenye maeneo hayo, ni ukweli usiopingika kuwa benki hii, haina uwezo wa kutoa mikopo inayohitaji kwa wale wenye nia ya dhati kukifanya kilimo kuwa cha kisasa, kibiashara na endelevu.

Mkopaji anapokwenda benki ya kilimo na wao baada ya kujihakikishia mhusika anastahili kupata mkopo, humpeleka moja kwa moja benki za kibiashara kama vile CRDB na National Microfinance Bank (NMB), ili aweze kupatiwa mkopo huo kwa masharti ya benki hizo.

Mteja anapaswa kuanza kujieleza upya. Anapaswa kuanza taratibu za kupata mkopo na pengine anaweza kushindwa kabisa kupata mkopo huo, kutokana na masharti ya dhamana kuwa makubwa na mlolongo mrefu.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa mkopo wa kilimo, ni tofauti na mikopo mingine. Mkopo huu, hauwezi kulinganishwa na mkopo wa kibiashara za kawaida na katika hilo, benki za kibiashara zimeshindwa kutofautisha mazingira na mahitaji kwa mikopo ya aina hizo mbili.

Katika udalali huu, benki ya kilimo “eti” wanamdhamini mteja huyo kwa asilimia 40 tu ya mkopo anaouhitaji.

Kwa dhana hiyo, kitendo cha benki ya kilimo, kuhamishia wadau wake benki nyingine za kibiashara, imeshindwa kuhudumia walengwa.

Benki za Biashara zinatoa sura kuwa Benki ya Kilimo, haina uwezo wa kuhudumia wakulima, bali ni dalali wa kukusanya wahitaji wa mikopo ya kilimo na kuwaelekeza kwenye benki washirika na benki hiyo.

Dhana nyingine ni kwamba Benki ya Kilimo, bado haijajiimarisha kiutendaji. Haina uwezo kimuundo na kimfumo wa kutoa mikopo.

Jambo hilo linatoa tafakuri kuwa serikali inatoa mtaji kwa Benki ya Kilimo na benki kwa makubaliano na benki washirika, inahamisha mtaji huo kwenda kwenye benki hizo na yenyewe kuishi kwa kamisheni.

Matokeo yake, kuna uwezekano wa riba ya mikopo kwa wakulima kupandishwa, tofauti na kwamba kama mikopo hiyo, ingetolewa na benki yenyewe.

Kutokana na muktadha huo, ni wakati muafaka sasa kwa serikali, kuelekeza Benki ya Kilimo, kufanya kazi zake, kutokana na malengo ya kuanzishwa kwa benki hiyo.

Katika uwekezaji mkubwa, dhamana ya mkopaji inatakiwa kuwa nini hasa? Ni ghorofa, trekta, magari au nini?

Kama mkulima anayo ardhi ya kutosha, ana wataalam wa kuendesha mradi husika na ana uhakika mikataba ya soko kwa mazao atakayozalisha na mazao hayo au mkopo huo una bima, ni kwanini asumbuliwe ama kuzungushwa hadi kukatishwa tama?

Waziri Mkuu Majaliwa aone umuhimu na kuhakikisha kuwa kama benki haina uwezo wa kutimiza hatua zote za mkopaji hadi anapatiwa mkopo wake, ni serikali ikaelekeza fedha hizo kwa mabenki ya kibiashara moja kwa moja.

Hii itasaidia kuondoa ukiritimba na udalali unaofanywa na Benki ya Kilimo, kwa kuwa utaratibu unaotumika sasa na benki hiyo, unamuumiza mkopaji na unasababisha baadhi ya wakopaji kushindwa kurejesha mikopo yao.

Ni kutokana na kuwapo kwa mlolongo mrefu unaosababisha mkopo kuchelewa kutoka kulingana na ratiba ya uzalishaji.

Vinginevyo, kilimo hakitakuwa na hivyo, malengo mahususi ya kuanzishwa kwa benki ya kilimo, yatakuwa yamepotea.

Tusione aibu kurekebisha pale ambapo tumeteleza kama taifa. Kilimo cha kibiashara kinahitaji uwekezaji mkubwa. Hauwezi kupatikana na mkulima mwenyewe. Anahitaji usaidizi wa mkopo au ruzuku.

Hebu tujiulize: Uwekezaji kwenye kilimo kisichotegemea mvua – greenhouse – kinaweza kufanywa na mwananchi wa kipato cha chini, bila msaada kutoka sekta za serikalini?

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Makala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Potofu huzaa potoshi/ potoshi huzaa potofu?

Spread the loveDayosisi 7 za KKKT katika kanda ya Ziwa na Magharibi,...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Rais Samia ni Mzanzibari: Shida Iko Wapi?

Spread the loveTAIFA linakabiliwa na upungufu wa fikra sahihi. Upungufu huu unaonekana...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Mpina mwiba CCM, ahofia kuzibwa mdomo

Spread the loveWAKATI Chama cha Mapinduzi (CCM), kikijinasibu kuwa kinara wa demokrasia...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Mabeyo ametuepusha

Spread the loveNIMEGUSWA na uadilifu, utiifu na uaminifu wa Mkuu mstaafu wa...

error: Content is protected !!