August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Benki ya BOA yatoa mafunzo kwa wafanyabiashara wa Mwanza

Mkurugenzi Mtendaji wa BOA Benki, Adam Mihayo, akifungua warsha ya kuwajengea uwezo wafanyabiashara wateja wa benki hiyo

Spread the love

 

BENKI ya Bank of Afrika -Tanzania (BOA) imeendesha warsha ya uwezeshaji kwa wajasiriamali iliyowalenga wafanyabiashara wadogo na wa kati (SME) ikiwa na lengo la kuwapatia ujuzi na maarifa juu ya muhimu wa ukuaji mzuri na thabiti wa biashara zao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).

Mafunzo hayo ambayo yamewashirikisha washiriki kutoka maeneo mbalimbali mkoani Mwanza, waliwajengewa uwezo kuhusu masuala ya kifedha ikiwemo mbinu za utunzaji fedha, namna ya kukuza mtaji na kushirikiana ili kukua pamoja kibiashara.

Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya BOA, Adam Mihayo, aliwahimiza wajasiriamali na wafanyabiashara nchini kuchangamkia huduma za kifedha zitolewazo na benki hiyo ili kuongeza tija.

“Sisi BOA benki katika mpango mkakati wa miaka mitatu ni kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi. Nawakaribisha Bank of Africa kwa kuwa ndiyo benki yenye mtazamo chanya unaolenga kuwasaidia wajasiriamali wadogo na wakati, hii ni katika huduma zetu madhubuti za ufunguaji wa akaunti ya benki, mikopo, ufumbuzi wa kibiashara na ushauri katika kukuza na kustawisha biashara za wajasiriamali. Karibuni tuwahudumie,” alisema, Mihayo.

Mkurugenzi huyo alisema kwa kipindi cha mwaka jana benki ilitoa mikopo ya kiasi cha Sh. 32 bilioni kwa wajasiriamali wadogo na wakati, ukilinganisha na mwaka huu mpaka mwezi Juni mwaka huu, tayari imeshatoa kiasi cha Sh 23 bilioni, ikiwa ni mwenendelezo mzuri na tunatumaini kwamba mpaka mwisho wa mwaka tutakua tumetoa kiasi kikubwa zaidi.

“Katika mpango mkakati wa miaka mitatu pia tumepanga kutoa mikopo ya kiasi cha Sh 132 bilioni kwa sekta hii nyeti na tunaamini katika kufanya hivyo tunachangia ukuaji wa uchumi wetu. Dhumuni kubwa la warsha hii ni kuwawezesha wafanyabiashara wa jijini Mwanza ambao ni wateja wetu katika maeneo mbalimbali.

“Tunaamini BOA, tunaendelea vizuri kibiashara. Ukiangalia mahesabu yetu tumeweza kukuza mizania yetu (balance sheet) mpaka kufikia Sh 711 bilioni, ukuaji ambao hatujawahi kufikia, faida yetu pia imekua kwa 37% ukilinganisha juni mwaka jana faida ya Sh 3.4 bilioni na Juni mwaka huu ya Sh 4.7 bilioni. Tunaendelea kuboresha huduma zetu ili kufikia mahitaji ya wateja wetu,” alisema Mihayo.

Baadhi ya wafanyabiashara waliohudhuria warsha hiyo, wameipongeza BOA, kwa namna ilivyowawezesha kwa njia ya mikopo na kuinua biashara zao ambapo wameomba benki hiyo kuendelea kuboresha zaidi huduma zake ili kuwanufaisha wafanyabiashara wengi zaidi.

Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo na kati wa BOA, Ninael Mndeme, amewahakikishia wafanyabiashara hao kwamba huduma za mikopo zitatolewa kwa wakati wote katika benki hiyo kwa kuzingatia kanuni za kibenki nchini.
error: Content is protected !!