December 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mkapa atikiswa, Benk M yafungwa

Spread the love

RAIS mstaafu Benjamin William Mkapa, ameaza “kuonja joto ya jiwe,” baada ya serikali kupitia Benki Kuu ya taifa (BoT), kuifuta rasmi benki ya Tanzania PLC, maarufu kama Benki M, ambayo inatajwa kuwa ni moja ya mali za kiongozi huyo. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Taarifa ya BoT iliyotolewa leo Jumanne kwa vyombo vya habari na Naibu Gavana, Dk. Bernard Kibese, inaeleza Benki M imefungwa kutokana na kushindwa kujiendesha na hivyo kuwa “mufilisi.”

Naibu Gavana Kibese anaeleza katika taarifa yake hiyo, kwamba “BoT imeamua kuhamisha mali, madeni na wafanyakazi wa iliyokuwa Benki M kwenda katika benki ya Azania, kutokana na benki hiyo kushindwa kujiendesha.”

Anasema, “maamuzi haya yamechukuliwa kufuatia uchunguzi uliofanywa na BoT ambao umegundulika kuwa Benki M imekumbwa na ukwasi mkubwa na imeshindwa kulipa madeni yake, zikiwamo amana za wateja.”

Kabla ya hatua hii, naibu gavana Kibise ameeleza kuwa BoT iliiweka benki hiyo chini ya uangalizi wake, tokea tarehe 2 Agosti mwaka jana.

Tokea kuondoka Ikulu (mwaka 2005), Mkapa amekuwa akihusishwa na umiliki wa Benk M. Mkapa hajawahi kukana madai hayo.

Sheria ya fedha imeipa mamlaka BoT kusimamia shughuli zote za kifedha nchini, ikiwamo kutoa leseni kwa mabenki na taasisi za fedha.

Bank M ilipewa leseni ya kufanya shughuli zake nchini mwaka 2008. Hadi inafungwa ilikuwa na matawi matano na mtaji wa Sh. 1 trilioni.

Kabla ya kuiweka chini ya uangalizi, BoT ilifanya mikutano ya mara kwa mara na menejementi ya benki hiyo kwa lengo la kuipa muda wa kurejesha mtaji na kulipia madeni inayodaiwa.

Benki hiyo ilikuwa na jumla ya matawi matano, matatu yalikuwa jijini Dar es Salaam na mengine mawili yalikuwa Arusha na Mwanza.

Katika kuhakikisha Benk M inajikwamua katika sakata la kufungwa, BoT ilitoa muda wa uangalizi wa siku 90, kuanzia 2 Novemba 2018 na baadaye ikaongozea muda wa mwingine wa siku 60. Hakuna hatua zilizochukuliwa.

BoT imetoa mamlaka kwa Azania Bank kuandaa taratibu za kisheria za kuhamisha mali na madeni yote ya Benk M kwenda benki hiyo.

Taarifa ya BoT imewataka wateja wote wenye amana na wadai wengine wa Bank M kuwa na subira na kwamba kila mteja ataarifiwa ni lini ataanza kupata huduma kupitia Azania Bank.

“Wale wenye mikopo wanatakia kuendelea kulipa mikopo yao kulingana na mikataba yao; BoT italisimamia jambo hili kwa karibu,” ameeleza naibu gavana Kibise.

Naibu gavana huyu anasema, maamuzi ya kuipeleka benki hiyo kwa benki ya Azania yanatokana na benki hiyo kuwa imara na kuwa mtaji mkubwa wa kiasi Sh. 164 bilioni. Mtaji unaotakiwa kisheria ni Sh. 15 bilioni.

error: Content is protected !!