July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Benki Kuu kupunguza fedha kwenye mzunguko kudhibiti mfumuko wa bei

Dk. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania imesema Benki Kuu nchini humo imelazimika kuanza kupunguza kiasi cha ukwasi inachoongeza kwenye uchumi ili kudhibiti hatari ya kuanza kuongezeka kwa kasi ya mfumuko wa bei nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Hayo yameelezwa leo Jumanne tarehe 14 Juni, 2022 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi yam waka 2021 na mpango wa maendeleo ya taifa wa mwaka 2022/23.

Dk. Mwigulu amesema hatua hiyo ni kutokana na kuanza kuongezeka kwa kasi mfumuko wa bei za mafuta na vyakula kufuatia athari za vita vya Ukraine.

Amesema “vita hiyo imeongeza changamoto ya kuvurugika kwa minyororo ya ugavi na kusababisha kuongezeka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, pamoja na bei ya vyakula kama ngano na mafuta ya kula na kuhatarisha kupanda zaidi kwa mfumuko wa bei.”

Awali Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania ilitekeleza sera ya fedha yenye lengo la kuongeza ukwasi katika uchumi, ili kuchochea ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi na kusaidia kuimarisha shughuli mbalimbali za kiuchumi zilizokuwa zimeathiriwa na janga la UVIKO-19.

Dk. Mwigulu amesema Benki Kuu ya Tanzania imekuwa ikitumia nyenzo mbalimbali za sera ya fedha kwa ajili ya kuongeza ukwasi katika sekta ya benki, ikiwemo kutoa mikopo ya muda mfupi kwa mabenki, kununua fedha za kigeni kwenye soko la jumla, na kuingia mikataba ya kubadilishana fedha za kigeni na mabenki (foreign exchange swap).

“Vilevile, Benki Kuu ilichukua hatua za ziada za kisera kwa ajili ya kuchochea ongezeko la mikopo nafuu kwa sekta binafsi, hususan shughuli za kilimo,” amesema.

Hatua hizo zinaonekana kuchangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei ambapo Mwaka 2021, mfumuko wa bei uliongezeka na kufikia wastani wa asilimia 3.7 kwa mwaka ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.3 katika kipindi cha mwaka 2020.

Aidha, Dk. Nchemba amesema mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 3.8 Aprili 2022 ikilinganishwa na asilimia 3.3 Aprili 2021.

error: Content is protected !!