January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Benjamin Mkapa: Tujadili sifa, tusijadili mtu

Rais Mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa

Spread the love

RAIS mstaafu Benjamin Mkapa, amejitosa katika kinyang’anyiro cha urais cha mwaka kesho. Amewekeza kwa waziri mkuu Mizengo Pinda.

Akizungumza katika harambee ya kuchangia fedha za mradi wa kusaidia maboresho ya sekta ya afya vijijini, Jumamosi iliyopita, Mkapa alisema, Pinda ni miongoni mwa viongozi wachache waadilifu ndani ya serikali.

Alisema, Pinda “amefanya kazi nzuri. Anakubalika kwa wananchi na amekuwa mfano wa kuigwa miongoni mwa viongozi waliopo madarakani.”

Harambee ambako Mkapa alimporomoshea sifa waziri mkuu huyo, iliandaliwa na taasisi ya Benjamin William Mkapa HIV/AIDS. Iliendeshwa na Pinda mwenyewe.

Katika hili la kutoa maoni yake katika kumtafuta mrithi wa Rais Jakaya Kikwete; au rais mwingine atakayekuja miaka mitano na hata 10 ijayo, Mkapa yumkini ana sura mbili.

Akiwa raia wa Jamhuri ya Muungano, Mkapa anayo haki ya kutoa maoni katika jambo lolote linalohusu taifa lake. Anayo haki ya kueleza kile kilichomo moyoni mwake.

Anaweza kukielekeza chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – ikiwa chama hicho kitapenda kupokea ushauri wake juu ya mgombea wanayeona anastahili kupeperusha bendera yao.

Aidha, yeye akiwa rais mstaafu – kwa sababu anaishi kwa kodi za wananchi – ana wajibu wa ziada wa kulikumbusha taifa lake juu ya masuala muhinu ya kusimamia. Hakuna shaka kuwa anao wajibu na haki hiyo.

Hata hivyo, kabla ya kutoa maoni yake katika suala zito kama hili; au kujitosa katika kumfanyia kampeni Pinda, Mkapa angeeleza – kwa maoni yake – rais ajaye anatakiwa kulifanyia nini taifa lake. Yapi majukumu yake ya msingi. Zipi changamoto. Yapi matatizo. Na aonyeshe njia zitakazoweza kutumika kutatua matatizo hayo.

Ni kama ilivyokuwa wakati wa uhai wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Alipojitosa kujadili mrithi wa Alli Hassan Mwinyi, Nyerere hakujadili mtu. Alijadili sifa za kiongozi anayetakiwa kumrithi Mwinyi. Lakini huyu Mkapa anajadili mtu. Hajadili sifa.

Nyerere alieleza matatizo yanayokabili taifa lake. Akasema, “…rushwa inanuka nchini.” Akataka kiongozi atakayekuja sharti awe mwadilifu. Aliyetayari kupambana na rushwa bila woga wala aibu.

Hivyo basi, changamoto kuu ya sasa, ni kutafuta mgombea urais ambaye atasimamia uadilifu wa kimfumo. Siyo uadilifu wa mtu binafsi.

Rais atakayekuja, ni sharti awe na ubavu wa kukabiliana na ufisadi na mafisadi. Awe na ujasiri wa kuzuia wizi wa mali ya umma; mikataba ya kinyonyaji; ujangili; dawa za kulevya na ufujaji kodi za wananchi.

Kiongozi anayetakiwa ni yule atakayekuwa tayari kutumia mamlaka ya umma kwa maslahi ya umma. Atakayefuata miiko na maadili ya uongozi. Yule ambaye hatatumia madaraka vibaya; au kutumia mamlaka ya umma kulipa fadhila.

Mathalani, kiongozi aliyepo sasa – Rais Jakaya Kikwete – mara baada ya kuingia ikulu, wengi alioteua walikuwa wanachama wa kundi lake la wanamtandao.

Hivyo basi, kitendo cha Mkapa kumpigia kampeni Pinda kwa kujadili mtu badala ya sifa, kinamuondolea fursa adhimu ya kushiriki kulitafutia taifa lake rais bora.

Sura ya pili ya Mkapa ni hii: Hana sifa ya kuwaambia wananchi, yupi ni rais bora na anayeweza kuwa sahihi kukabiliana na matatizo yaliyopo. Kwanini? Kwa kuwa naye hana sifa ya uandilifu.

Ikiwa Nyerere aliyekuwa msafi aliaminisha wananchi kuwa “Mkapa ni Mr. Clean”- Bw. Msafi, lakini ghafla aliyeitwa msafi akawa “mchafu,” Mkapa aliyechafuka hawezi kumjua msafi.

Aliyeitwa msafi, ndiye aliingia Ikulu na kuanza kutelekeza usafi. Akaanzisha kampuni ya biashara – ANBEM Co. Limited – kwa kutumia rasimali za umma.

Akabinafsisha mashirika ya umma, mithili ya shamba lisilo na mwenyewe.

Akaruhusu na, au kunyamazia ukwapuzi wa mabilioni ya shilingi serikalini na ndani ya Benki Kuu ya taifa (BoT).

Miongoni mwa fedha zilizoibwa, ni pamoja na zile zilizochotwa kupitia akaunti ya madeni ya nje (EPA), katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2005.

Hapa ndiko kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd., ilipewa “zawadi” ya kiasi cha Sh. 70 bilioni kati ya Sh. 130 bilioni zilizochotwa BoT.

Ushahidi juu ya Mkapa kushiriki au kunyamazia wizi katika akaunti ya EPA, uliwekwa hadharani na Bhyidinka Michael Sanze, wakili katika kampuni ya mawakili ya Malegesi Law Chambers ya Dar es Salaam.

Sanze ndiye alishuhudia mkataba kati ya Kagoda na serikali. Wakili huyo anakiri kuwa ni yeye aliyeshuhudia mikataba ya Kagoda na makampuni mengine ya nje.

Mbali na fedha zilizoibwa katika akaunti ya EPA, mabilioni mengine ya shilingi yalikwapuliwa na makampuni ya Tangold Limited, Deep Green Finance Limited, Meremeta na Mwananchi Gold Ltd.

Hakuishia hapo. Ni Mkapa aliyeingiza nchini kampuni ya kigeni kutoka Afrika Kusini – Net Group Solutions – ili kuikabidhi shirika la umeme la taifa (Tanesco), kuvuna wasichopanda.

Kazi ya Net Group ndani ya shirika la umma, haikuwa kuzalisha; kuwekeza mtaji; au kutafuta vyanzo vipya vya umeme. Kazi ya kampuni ya “makaburu’ ilikuwa kukusanya mapato na kukamua wananchi.

Katika kipindi cha miaka saba ya mkataba kati ya serikali na Net Group, Tanesco ikashindwa kuzalisha umeme unaoendana na mahitaji. Ikashindwa kuwekeza katika miradi mipya ya umeme.

Matokeo yake, miundo mbinu ya umeme ikachakaa. Taifa likatumbukia katika giza la milele na milele. Tanesco iliyokuwa imara, haraka ikatumbukia katika mikataba ya kinyonyaji ya kuzalisha umeme wa dharula.

Tanesco iliyokuwa inajiendesha kwa faida, ikatumbukia katika madeni makubwa yanayohatarisha hata uhai wa shirika lenyewe.

Miongoni mwa mikataba ya kinyonyaji ambayo imefungwa kutokana na shirika kutafunwa na kampuni iliyoletwa na Mkapa, ni pamoja na mkataba wa kinyonyaji wa kuzalisha umeme wa Richmond na dada yake Dowans.

Makampuni mengine, ni Aggreko; Symbion; Songas na “ndoa ya mkeka” iliyofungwa kwa mara ya pili kati yake na kampuni ya Independent Powel Tanzania Limited (IPTL).

Mkataba wa kwanza kati ya IPTL na serikali ulifungwa Septemba 1994. Katika mkataba huu, serikali ilijifunga kulipa IPTL kiasi cha Sh. 6 bilioni kwa mwezi kwa umeme usiokuwepo.

Januari mwaka huu, mkataba mpya kati ya Tanesco na IPTL kupitia anayeitwa mmiliki mpya, kampuni ya Pan African Power Solutions (PAP), ulifungwa katika mazingira yaliyosheheni utata.

Taarifa zinasema, mkataba kati ya Tanesco na PAP, hauna tofauti yoyote kubwa na mkataba kati ya Tanesco na IPTL.

Ni Mkapa na utawala wake waliobinafsisha mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya na kuumilikisha kwa watu waliokaribu na rais. Bunge la Jamhuri lilielezwa na Mtendaji Mkuu wa Kiwira Coal and Power Limited (KCP), Francis Tabaro, kuwa mgodi huo ulikuwa ukimilikiwa na watu walio karibu na Mkapa.

Waliotajwa kwa mujibu wa taarifa hizo, ni mtoto wa kuzaa wa Benjamin Mkapa, Nick (Nicholas) Mkapa na mkewe Foster Mkapa. Hawa wanamiliki kampuni ya Fosnik Enterprises, moja ya makampuni yanayomiliki mgodi.

Mkurugenzi mwingine ambaye pia ni mmiliki ametajwa kuwa ni D. Maembe.

Kampuni ya Mkapa ni miongoni mwa makampuni manne yaliyoungana na “kumilikishwa” mgodi wa Kiwira ambao ulikuwa mali ya serikali kwa asilimia 100. KCP ilianzishwa Julai 2005.

Si hayo tu. Akiwa ikulu ya magogoni, Mkapa alimpa mkewe, Anne Mkapa, mamlaka ya kukusanya fedha na kuendesha kinachoitwa, “Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote” (EOTF). Akautumia mfuko huo, kujilimbikizia mali nyingi.

Hadi wanaondoka ikulu, siyo Mpaka wala mkewe, aliyesema fedha za kuendesha mfuko ya EOTF zilitoka wapi. Mafanikio yaliyofikiwa wala hesabu za mfuko ni siri yao.

“Mfuko wa Mama Mkapa,” ulianzishwa mara baada ya Mkapa kuingia madarakani, Novemba 1995. Kwa muda wote ambao Mkapa alikuwa ikulu, mfuko huu ulikuwa unaendeshea shughuli zake katika majengo ya Ikulu.

Hata gharama za bili ya maji, umeme, simu na mishahara ya wafanyakazi vililipwa na serikali. Misaada na michango iliyotolewa na wafadhili, mingi ilitolewa kwa kuwa mwenyekiti wake ni mke wa rais. Mfuko uligeuka, ingawa siyo rasmi, kuwa wa umma.

Hakika, kuna mengi yamefanyika chini ya utawala wake. Ameingiza nchi katika mikataba ya kinyonyaji katika uchimbaji madini katika maeneo mbalimbali nchini, ukiwamo mgodi wa Tulawaka, Bulyanhulu, North Mara na Geita Gold Mine.

Ameuza nyumba za serikali. Naye akajimilikisha baadhi ya nyumba hizo. Akaruhusu waziri wake, John Pombe Magufuli, naye kujimilikisha.

Akasimamia uuzaji unaofanana na utoaji bure mashirika ya umma, ikiwamo “utoaji bure” iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC). Benki iliyokuwa na matawi nchi mzima na mtaji kedekede, iliuzwa kwa bei ya kutupwa kwa benki ya ABSA ya Afrika Kusini.

Leo hii, NBC iliyoelezwa inauzwa kwa watu wenye uwezo wa kuiendesha kuliko wazalendo waliopo, iko hoi kibiashara. Imepoteza mtaji; na sasa inaendeshwa kwa hisani ya BoT.

Ni Mkapa aliyeuza shirika la ndege la taifa (ACT); migodi na mashamba.

Katika muktadha huo, mtu mwenye yote haya, anapata wapi uhalali na ujasiri wa kutupendekezea mtu ambaye anadai ni mwadilifu? Mtu mwenye viwango vya chini vya uadilifu kama Mkapa, anawezaje kumjua mwadilifu wa dhati? Hawezi.

Ni bahati njema kuwa Nyerere alifariki dunia kabla Mkapa hajamaliza ngwe yake ya kwanza ya uongozi, Oktoba 2010. Vinginevyo, asingeruhusu Mkapa kushika madaraka kwa vipindi viwili mfululizo. Nyerere alifariki dunia 14 Oktoba 1999.

Taarifa zinanukuu baadhi ya viongozi waandamizi nchini wakisema, Nyerere alikuwa amejiapiza kumzuia Mkapa kuwa rais kwa kipindi cha pili. Alimchoka.

Hivyo basi, tukimjadili Mkapa na yule anayempigia chapuo, tunawaona wana sifa moja inayofanana. Wote wawili hawaheshimu utawala wa sheria. Ni wababe.

Mara mbili, Pinda aliagiza ndani ya bunge vyombo vya dola kuchukua sheria mkononi. Mara ya kwanza, ni pale alipoagiza watuhumiwa wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi – Albino – wauawe.

Mara ya pili ni pale Pinda alipoagiza kupigwa kwa wananchi waliokuwa wanatekeleza matakwa yao ya kikatiba kupinga mradi wa gesi kwenye mikoa ya Kusini, wakisema hautawanufaisha – kama ilivyo kwa wanaoishi katika maeneo au karibu na migodi ya dhahabu na alimamsi.

Katika kipindi cha utawala wake, Mkapa aliruhusu vyombo vya dola – jeshi la polisi; vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) vya Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU); Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM) na makundi mengine ya Janjaweed – kuendesha mauaji makubwa katika Visiwani Pemba na Unguja, 26 na 27 Januari 2001.

Katika tukio hilo lililoweka doa baya taifa hili, wanakaokadiriwa kati ya watu 30 na 75 waliuawa.

Sifa nyingine ambayo Pinda anayo, ni kutojiamini. Yawezekana hiyo ndiyo iliyomsukuma Mkapa kumuunga mkono kutimiza ndoto zake.

Anajua ikiwa Pinda atafanikiwa kuwa rais, atamburuza. Atamyumbisha. Anajua chini ya Pinda machafu yake yatalindwa. Nje ya hapo, Mkapa hana kingine cha kumsifia Pinda.

Tusikubali kuruhusu kuchaguliwa mgombea, kabla ya kukubaliana juu ya sifa za rais tunayemhitaji.

error: Content is protected !!