May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Beki Stars atundika daluga, kuagwa Januari 10

Aggrey Morris

Spread the love

BEKI mwandamizi wa Azam FC, Aggrey Morris ametangaza rasmi kustaafu kuitumikia timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ akiwa na umri wa miaka 37 na kuagwa rasmi kwenye mchezo wa kirafiki kati Taifa Stars dhidi ya Congo utakaochzwa tarehe 10 Januari, 2021 kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Aggrey Morris ambaye amedumu katika kikosi hicho kwa miaka 11, atakumbukwa kama moja ya wachezaji waliofunga bao kwenye ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Uganda uliofanikisha Taifa Stars kufuzu Fainali za kombe la mataifa Afrika ‘AFCON’ nchini Misri 2019.

Taarifa ya kutundika kwake daluga zimetolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo tarehe 5 Januari, 2021 na kueleza utaratibu mzima utakaotumika kumuaga mchezaji huyo mwandamizi kwenye kikosi hiko kwa sasa.

Mchezaji huyo ambaye ni mzaliwa wa visiwani Zanzibar, aliitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha timu ya Taifa 2010 na kufanikiwa kucheza michezo 35 ya kimataifa na kufunga mabao mawili, huku kwa upande wa kikosi cha timu ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ alicheza michezo 15 na kufunga mabao sita.

Kwa sasa mchezaji huyo amejumuishwa kwenye kikosi cha Tifa Stars ambacho kipo kambini kujiandaa na michuano ya Kombe la mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani ‘CHAN’ ambapo ataagwa rasmi kwenye mchezo huo wa kirafiki.

Mara baada ya kuagwa mchezaji huyo atakuwa na majukumu ya kuitumikia klabu yake ya Azam FC ambayo alijiunga nayo toka 2009 akitokea klabu ya Mafunzo inyoshiriki Ligi Kuu Zanzibar.

error: Content is protected !!