May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bei mpya za mafuta zapigwa ‘stop’ Tanzania

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania imetangaza kusitisha bei mpya za mafuta zilizokuwa zianze kutumika leo Jumatano, tarehe 1 Septemba 2021. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Bei hizo za mafuta ya taa, petrol na diseli zilitangazwa jana Jumanne tarehe 31 Agosti 2021 na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura).

Kila Jumatano ya mwezi, Ewura hutangaza bei mpya ambapo huwa na kawaida ya kupanda, kushuka au kubaki kama zilivyo. Kwa mwezi huu wa Septemba, zilikuwa zimepanda.

Kutokana na kupanda huko, Serikali imewaita bungeni viongozi wa Ewura na kutoa maagizo ya kusitisha bei hizo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Godfey Chibulunje akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma amesema, Serikali imeunda timu maalum ya kupitia bei hizo.

“Jana tulitangaza bei mpya za mafuta zilizokuwa zianze kutumika leo Jumatano tarehe 1 Septemba. Kutokana na mabadiliko hayo ya bei, tumepata maelekezo mahususi kwamba bei hizo zisitishwe na ziendelee kutumika bei zilizokuwepo za ,” amesema Chibulunje.

“Serikali imeunda timu maalum ya kupitia mapitio kuangalia bei zinavyopangwa na kuangalia viashiria mbalimbali vya kwenye bei na bei hizi zitaendelea kutumika hadi timu hiyo itakapomaliza kufanya kazi yake na tutatoa maelekezo mapya,” amesema.

Amesema, timu hiyo inajukuisha watu kutoka wizara ya nishati, Ewura, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja, wizara ya fedha na taasisi zingine.

Chibulunje amesema, timu hiyo haijapewa muda maalum wa kufanyia kazi suala hilo.

error: Content is protected !!