August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Begi la Gwajima utata-Shahidi

Spread the love

ACP Pamphil Mholery, Ofisa wa Jeshi la Polisi, Kitengo cha Utawala Kanda Maalum ya Dar es Salaam ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa, begi la Mchungaji Josephat Gwajima, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima lilikuwa na shaka, anaandika Faki Sosi.

Katika ushahidi uliotolewa jana mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha, Shadrack Kimaro, Wakili wa Serikali Mwandamizi amedai kuwa, shauri hilo limetajwa ili kuendelea na hatua ya usikilizwaji.

Mholery ameeleza mahakama kwamba, anakumbuka siku ya tarehe 29 Machi mwaka jana, alikuwa katika majukumu yake kama Ofisa wa Zamu Mkoa wa Kinondoni, alipokea amri kutoka kwa mkuu wake akimtaka aende Hospitali ya TMJ.

“Baada ya kupata taarifa hiyo, niliondoka saa tisa usiku na baadhi ya maofisa wenzangu, tulipofika tulikutana na kundi la watu, ambapo tuliwataka watoke nje ya hospitali kwani walionekana tishio,” amesema.

Akitoa ushahidi huo kwa mfumo wa kujibu maswali kutoka kwa Wakili Kimaro, Mholery ameeleza baada ya kuwatoa nje, walipandisha kwenye wodi aliyolazwa Gwajima ambapo walikutana na watu wengine watatu.

Watu hao aliowakuta ni msaidizi wa askofu huyo, Yekonia Bihagaze (mshtakiwa wa pili), mfanyabiashara George Mzava (mshitakiwa wa tatu) na mkazi wa Kimara Baruti, Geofrey Milulu (mshitakiwa wa nne).

Badaa ya kukutana na watu hao, ofisa huyo alidai aliwauliza wamefuata nini, usiku katika hospitali hiyo, ndipo walipomjibu kuwa, wamefika kumuona mgonjwa (Gwajima).

“Mmoja wao ambaye ni mshtakiwa wa pili alikuwa ameshika begi la kijani, ambalo tuliwekea shaka kwamba imekuaje watu hao kubeba begi usiku,” ameeleza.

Kutokana na hofu hiyo, shahidi alidai walilazimika kulifanyia uchunguzi begi hilo ambapo walibaini kuwepo kwa vitu kadhaa ikiwemo silaha aina ya Beretta namba CAT 5802 , risasi tatu za pisto na risasi 17 za shotgun.

“Hapo tulipata tena shaka kwanini begi lina silaha tena usiku, hivyo tukashindwa kujua kwamba imekuaje waliokuja kumuona mgonjwa na silaha kwenye begi,” ameeleza Mholery.

Ameeleza kuwa, katika upekuzi huo bastola hiyo ilitolewa na kukutwa ikiwa na risasi tatu ndani yake.

Ofisa huyo, ameeleza kuwa aliamuru watu hao kuwekwa chini ya ulinzi kisha kuwafikisha Kituo cha Polisi kwa ajili ya mahojiano.

Mara baada ya kutoa ushahidi, aliiomba mahakama kupokea nyaraka iliyokuwa na orodha ya vitu vilivyokuwa kwenye begi la Gwajima. Hata hivyo upande wa utetezi kupitia wakili Peter Kibatala uliiomba mahakama kuitupilia mbali nyaraka hiyo.

Kibatala ameimbia mahakama kuwa, nyaraka hizo haziuhusiani kabisa na kesi iliyopo mahakamani kulingana na kosa linalomkabili mshtakiwa.

Amedai kuwa, hakukuwa na uhusiano wowote baina ya vitu vilivyo orodheshwa kwenye nyaraka hiyo, pamoja na kile alichokiongea hivyo mahakama isipokee.

Hata hivyo, Hakimu Mkeha amesema mahakama imepokea kithibitisho hicho kutokana na mahusiano na kesi iliyopo.

Hakimu Mkeha amesema hatua hiyo inatokana na mambo makuu matatu hususan mashtaka, hivyo hata shahidi aliyoyatoa yanahusiana nayo.

Mara baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, Wakili Kibatala alimuuliza maswali kadhaa shahidi huyo lakini alionekana kushindwa kujibu.

Moja ya swali ambalo lilisababisha watu wacheke, Kibatala alimuuliza shahidi huyo kwamba ni ofisa gani aliyekuwa akichunguza makosa ya washtakiwa hao, alijibu hajui.

Shahidi huyo alikiri mbele ya mahakama kuwa, mshtakiwa wa tatu na wanne hawakukutwa na silaha bali waliunganishwa kutokana na kuwepo eneo la tukio.

Amesema kuwa, hata chumba alichokuwa amelazwa mshtakiwa wa kwanza Gwajima alikuwa hajui kama kilikuwa ni chumba cha ICU ama la.

Mara baada ya kutoa ushahidi huo, upande wa Jamhuri uliiomba mahakama kuahirisha usikilizwaji wa shauri hilo ili waende msibani. Hakimu Mkeha aliahirisha shauri hilo hadi Juni 2, mwaka huu.

Katika kesi hiyo inadaiwa kati ya Machi 27 na 29, mwaka jana jijini Dar es Salaam, Gwajima alishindwa kuhifadhi silaha aina ya Beretta namba CAT 5802 , risasi tatu za pisto na risasi 17 za shotgun.

Shitaka la pili na la tatu linawakabili washtakiwa waliobaki ambao wanadaiwa kwamba, Machi 29, mwaka jana katika Hospitali ya TMJ Mikocheni ‘A’ walikutwa wakimiliki silaha na risasi hizo bila ruhusa kutoka mamlaka husika.

error: Content is protected !!