July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

BBIO yatambulisha tuzo mpya

Spread the love

ASASI binafsi ya Broad Based Interest Organization (BBIO) inayoratibu mradi wa unaohamasisha na kuimarisha juhudi za utekelezaji mikakati ya maendeleo (AMAN), imetambulisha tuzo zinazolenga ujumbe na dhamira inayobebwa na kazi mbalimbali za tasnia ya muziki, filamu na habari nchini. Anaandika Regina Mkonde …. (endelea).

Tuzo hizo zimejikita kwenye vipengele vitatu ambavyo ni Tuzo za Muziki za Aman (Aman Music Award), Tuzo za Filamu za Aman (Aman Film Award) na Tuzo za Habari za Aman (Aman Media Award) pia tuzo hizo zitakuwa kwenye makundi mbalimbali kulingana na kazi zake.

Vigezo vya ushindani wa tuzo za Aman ni umahiri katika kutoa, kueneza na kufikisha ujumbe wa maendeleo kupitia muziki na filamu, ujumbe huo lazima uwe sawia na dira za maendeleo. Wananchi watahusika kupigia kura dhamira iliyobebwa na kazi mbalimbali kwenye kila kipengele.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Katibu Mtendaji wa BBIO, Amani Joram Mgullo amesema kuwa wazo la utoaji wa tuzo za amani limekuja baada ya Tanzania na mataifa mengine kuzindua mkakati mpya wa maendeleo.

Mkakati huo unalenga kutengeneza maisha bora na dunia bora kwa kila mtu ulimwenguni kote, pia umeainisha maeneo matano kuwa ya msingi katika kufanyiwa kazi ili kufikia adhma yake. Maeneo hayo ni watu, ustawi, amani, mazingira na ushirikiano.

“Mkakati wa maendeleo umeweka malengo 17 yanayotakiwa kutimizwa ifikapo mwaka 2030, mikakati mingi iliyotangulia imekuwa haifikii malengo na kusababisha jamii nyingi kuendelea kuishi kwenye hali duni zinazozidi kuzorota kila uchao,” amesema Mgullo na kuongeza:

“Juhudi za ushawishi na uwezeshaji zenye ufanisi zinatakiwa ili mkakati huu wa maendeleo endelevu uweze kufikia malengo yake. Tafiti zimethibitisha kuwa tasnia za muziki na filamu kupitia vyombo vya habari zinauwezo wa ushawishi na uwezeshaji na kuwafikia watu wa rika zote.”

Mgullo amedai kuwa, mradi wa aman kupitia tuzo za aman utasaidia kuchochea mapinduzi kwenye umahiri wa kutoa, kueneza, na kufikisha ujumbe wa maendeleo kupitia tasnia hizi maarufu.

Lengo la tuzo hizi ni kuchangia katika kuhakikisha dhima ya maisha bora na dunia bora kwa kila mtu inafikiwa.

Wananchi wametakiwa kushirikiana na asasi katika kusambaza mapinduzi yanayolenga kuunga mkono serikali katika juhudi zake za dhati za kuleta maendeleo kwa Taifa letu.

error: Content is protected !!