July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bay Port yalalamikiwa

Spread the love

BAADHI ya watumishi wa serikali wameilalamikia taasisi ya kutoa mikopo ya Bay Port kwa madai ya kuwaingiza watumishi hao katika mfumo wa kuomba mikopo bila ridhaa yao, anaandika Dany Tibason.

Mbali ya malalamiko hayo, pia wamelalamikia mikopo hiyo kuwa na riba kubwa.

Mmoja wa watumishi aliyelalamikia taasisi hiyo ni Masura Nyakarungu, Daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma ambaye amedai ameingizwa katika mkopo mkubwa na taasisi hiyo bila makubaliano.

Kwa mujibu wa Dk.Nyakarungu, taassi hiyo iliwahi kutoa semina kwa watumishi lakini bila yeye kuomba mkopo, aliingizwa katika mkopo wa Sh. 3,000,000 ambapo riba yake ilikuwa asilimia 30.

“Kutokana na semina hiyo niliandika barua kwa wakala na kuomba mkopo wa Sh. 1 Milioni,” amesema na kuongeza;

“Lakini cha kusikitisha waliniingizia kiasi cha milioni 3 kwenye akauti yangu badala ya Sh. 1 milioni niliyoomba, hata hivyo baada ya kuingiziwa kiasi hicho bila kuwa na makubaliano, nilianza kukatwa mshahara wangu ambapo mkopo uliwekewa riba ya asilimia 300 sawa na Sh. 9 milioni.

Raphael Kalinga, Meneja wa Bay Port Kanda ya Kati alikiri kuwepo kwa malalamiko hayo.

Kalinga amesema, “ni kweli Dk.Masura Nyakarungu aliingiziwa mkopo wa Sh. 3 Milioni kimakosa na hiyo ilitokana na utapeli ambao ulifanywa na mmoja wa wafanyakazi wa taasisi yetu.”

Amesema, mwombaji wa mkopo katika taasisi hiyo aandiki barua ya kuomba mkopo bali hujaza fomu za kuomba na hicho ndicho kilichofanywa na mmoja wa wafanyakazi wa taasisi hiyo ambaye hakuwa mwaminifu. Hata hivyo, Kalinga amesema, mfanyakazi hiyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi.

error: Content is protected !!