BARAZA la Wanawake la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA), limemtaka Rais Samia Suluhu Hassan asikatishwe tamaa na baadhi ya watu wanaopinga msimamo wake wa kukamilisha mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya, pamoja na tume huru ya uchaguzi, kabla ya 2025. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kilimanjaro … (endelea).
Wito huo umetolewa leo tarehe 8 Machi 2023, Kilimanjaro na Katibu MKuu wa Bawacha, Catherine Ruge, katika maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani, yaliyoandaliwa na Bawacha, ambapo mgeni rasmi ni Rais Samia.
“Tunatambua unafanya jitihada nyingi kwa kushirikiana na Mbowe kuhakikisha tunapata katiba mpya na tume huru ya uchaguzi kabla ya 2025, usiogope hujuma za wanaotaka ushindwe kama wao walioshindwa huko nyuma. Ukichunguza vizuri hata hao wanaopinga dhamira yako kupata katiba, hawakupingi bali wanakupima. Ni wakati wako kuandika historia ambayo itasomwa vizazi vijavyo,” amesema Ruge.
Ruge amesema kuwa, licha ya mchango mkubwa ambao wanawake wanatoa katika ujenzi wa Taifa, lakini hauendani na hali zao kimaisha.
“Rais naomba nikukumbushe,kwa mujibu wa takwimu za sensa zinaonyesha kwamba wanawake ni jeshi kubwa, tuko milioni 31. Ukubwa wetu sio tu kwa wingi wa idadi bali kwa kodi tunazolipa katika taifa hili na mchango tunaotoa katika taifa hili, lakini hadhi ya kina mama na watoto wa taifa hili haifanani na mchango wanaotoa,” amesema Ruge.
Ruge amesema “wanawake tunaishi maisha duni, hatuna uhakika kama unalitambua hilo, kule kwenye chama chako inawezekana wanawake wenzetu wa CCM hawakuambii ukweli wanakwambia mambo unayopenda kusikia kama mama anaupiga mwingi hata mahali walipostahili kukueleza changamoto uweze kuzitatua.”
Mwanasiasa huyo amesema Bawacha linatambua kazi nzuri inayofanywa na Rais Samia, lakini aendeleze jitihada za kutatua changamoto zinazowakabili wanawake nchini.
Leave a comment