Thursday , 30 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Bawacha wajipanga ‘kuwazika’ Mdee na wenzake
Habari za SiasaTangulizi

Bawacha wajipanga ‘kuwazika’ Mdee na wenzake

Halima Mdee
Spread the love

 

BARAZA la Wanawake la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA), linapanga mkakati mzito unaolenga kumzika kabisa kisiasa, aliyekuwa mwenyekiti wao wa taifa, Halima James Mdee. Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa kutoka ndani ya Chadema zinasema, wanawake wa chama hicho, wanapanga “kumalizana na Mdee,” wakati wa maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani, yaliyopangwa kufanyika kitaifa, mkoani Iringa.

Mtoa wa MwanaHALISI Online anasema, wanawake wa Chadema, wamekuwa wakihamasishana kujitokeza kwa wingi kwenye maadhimisho hayo, ili kuudhihirishia ulimwengu na baadhi ya viongozi wakuu wa chama hicho, kuwa “Bawacha bila Mdee, inawezekana.”

Mdee na wenzake 18, walifukuzwa uanachama wa chama hicho, tarehe 27 Novemba 2020, kufuatia kutiwa hatiani kwa makosa ya utovu wa nidhamu, usaliti, kuhujumu chama, upendeleo, kutengeneza migogoro; na  kushirikiana na wanaokitakia mabaya chama.

Mashitaka mengine, ni pamoja na kughushi nyaraka za chama na kwenda bungeni kujiapisha, kinyume na maekelezo na maamuzi ya chama chenyewe.

Wengine waliofukuzwa Chadema, ni waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu, Ester Bulaya na Esther Matiko; aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega; aliyekuwa Makamu Mwenyekiti baraza hilo (Bara), Hawa Subira Mwaifunga; aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bawacha (Bara), Jesca Kishoa; aliyekuwa katibu mwenezi, Agnesta Lambat na naibu katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar, Asia Mwadin Mohamed.

Mbali na viongozi hao wa Bawacha, Kamati Kuu ya chama hicho, iliyokutana jijini Dar es Salaam, chini ya mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, iliwavua uanachama, aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje na aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo.

Katika orodha hiyo, yupo pia Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba,  Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.

Mdee anatajwa kuwa ndiye kinara wa kundi hilo, lililopachikwa jina la Covid-19, katika mpango wa “usaliti ndani ya Chadema.”

Anatuhumiwa kushirikiana na Tendega, Bulaya, Agnesta na Kunti, kupeleka majina Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Bunge, ili hatimaye wateuliwe na kuapishwa kuwa wabunge.

Katika kutekeleza mradi huo, Mdee anaoenakana kuongea na baadhi ya viongozi wandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bunge, NEC, pamoja na baadhi ya watu walioko “kwenye mfumo,” ili kufanikisha dhuluma dhidi ya wanawake wa Chadema.

Devota Minja, Mwenyekiti wa Bawacha mkoa wa Morogoro

Hatua ya Mdee kuwafanya baadhi ya maswahiba zake kuwa wabunge, imewanyima fursa wanachama wa chama hicho wenye sifa zaidi ya “waliobebwa na Mdee” nafasi ya kuwa wabunge.

Wengi walioumizwa na hatua hiyo, ndiyo wanaohamasishana kukutana Iringa, “ili kuonyesha Bawacha ni kubwa kuliko mtu.”

Madai haya yanapata nguvu zaidi, kufuatia hatua ya serikali kumuachia huru Nusrat Hanje, kutoka gereza la Isanga, mkoani Dodoma, alikokuwa akishikiliwa kwa zaidi ya siku 140.

Nusrat, aliachiwa kutoka gerezani, usiku na siku ya tarehe 23 Novemba 2020 – siku moja kabla ya Mdee na kundi lake, kuapishwa na Spika Job Ndugai kuwa wabunge, katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma.

Katika maelezo yake, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga alisema, Nusrat na wenzake waliachiwa huru, baada ya Jamhuri kuona haina tena nia ya kuendelea na kesi.

Nusrat hakuwa miongoni mwa wanachama wa Chadema walioshiriki mchakato wa ndani wa chama hicho, katika kuwatafuta wabunge wake wa viti maalum.

Catherine Ruge

Aidha, Mdee na wenzake, wameapishwa kuwa wabunge, bila kujaza fomu Na. 8(d) wanayopaswa kujaza wabunge wa Viti Maalumu.

Kifungu C katika fomu hiyo, kinataka kuwapo uthibitisho wa vyama kutoka kwa katibu mkuu au naibu wake, pamoja na mhuri wa chama husika.

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, alinukuliwa akisema, “fomu Na.8(d) nilizoletewa na NEC bado ziko ofisini kwangu.”

Akaongeza, “NEC itueleze hawa imewateuaje bila kujaza hizi fomu ambazo bado ninazo?”

Mdee na wenzake 18, hawakujaza fomu hizo, hawakugonga mhuri, wala hawakwenda mahakamani kula kiapo, wakati hayo ni miongoni mwa masharti yanayopaswa kutekelezwa kwa mtu anayetaka kuwa mbunge.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa wa MwanaHALISI Online, katika mkakati wa kummaliza Mdee kwa kumuonyesha chama hicho ni taasisi iliyokamilika, wanawake hao wa Chadema, wameanza kuchangishana fedha kutoka mifukoni mwao, ili kuhakikisha maadhimisho hayo ya Iringa yanafana.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

“Ni utamaduni wetu kuadhimisha siku hii kila mwaka. Pamoja na kuhudhuria maadhimisho yanayoandaliwa ya umma, sisi kama chama cha siasa, tumekuwa tukiendesha makongamano mbalimbali, ambayo yamekuwa yakifana sana,”  anaeleza kiongozi mmoja wa Bawacha, ambaye ni mjumbe wa kamati tendaji.

Anasema, “wakati Mdee akiwa mwenyekiti wetu, alikuwa ndiye anayetuongoza. Safari hii, tumejipanga na wanachama wetu wameitikia wito wa kwenda Iringa, ili kumhakikishia yeye na wale wanaomtumia, kwamba Bawacha iko imara na inaweza kuwa imara zaidi bila yeye.”

Kwa mujibu wa mtoa taarifa huyo, wanachama kadhaa wa Bawacha na hata wale wasiokuwa wanachama wa baraza hilo, wameanza kuchangia majimbo yao, ili yaweze kukusanya wanawake na kuwafikisha Iringa.

Mathalani, mwenyekiti wa Chadema katika jimbo la Segerea, jijini Dar es Salaam, Patrick Asenga amesema, wanachana na viongozi wa jimbo hilo, wameanza michango itakayowezesha kupatikana kwa zaidi ya Sh.1.2 milioni, zitakazotumika kupeleka wanawake katika tamasha hilo.

“Hapa kwangu, tunatafuta zaidi ya Sh.1.2 milioni ili zisaidie wanawake kwenda Iringa. Hamasa ni kubwa sana,” amesema na kuongeza, “lakini mengi zaidi, wasiliana na viongozi wa Bawacha wenyewe watakuambia.”

Aidha, Bawacha wametoa tangazo mahususi kwa wanachama wake, kufurika Iringa, tarehe 8 Machi 2021.

Mdee alikuwa mmoja wa wabunge mahiri wa Chadema katika kipindi cha miaka 15 alichokuwa bungeni. Kabla ya kuwa mbunge wa Kawe, Dar es Salaam ambako aliliongoza jimbo hilo kati ya mwaka 2010 hadi 2020, alianzia Viti Maalum mwaka 2005.

Ndani ya kipindi hicho, Mdee amepitia dhoruba mbalimbali, ikiwamo kuhukumiwa kifungo au faini; kusimamishwa kuhudhuria mikutano ya Bunge, kushitakiwa Kamati ya Maadili ya Bunge na mahakamani na kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara jimboni kwake.

Hata hivyo, hatua ya kufukuzwa kwake uanachama wa Chadema, kumeanza kummomonyoa kisiasa na sasa taratibu waliokuwa wakimuita, “Mfalme wa Kawe na rais wa marais,” wanamshughulikia usiku na mchana kwa kile wanachoita, “matunda ya dhambi ya usaliti.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

TEMESA iliyokarabati Kivuko kwa Bil 7.5 yapata hati chafu

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

ACT-Wazalendo yakusanya Mil 8.5/- kodi ya zuio na kutokomea nazo

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

DC Kasilda Mgeni ahamasisha chakula shuleni

Spread the love  MKUU wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni...

Habari za Siasa

Bilioni 223.9 zapelekwa Tunduru ndani ya miaka 2 ya SSH

Spread the love  ZAIDI ya Sh. bilioni 223.9 zimepelekwa Wilaya ya Tunduru...

error: Content is protected !!