July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

BAVICHA wamuasi Mbowe, waapa kwenda Dodoma

Spread the love

BARAZA la vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), limeapa kwenda mkoani Dodoma kusaidia jeshi la polisi kuzuia mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaandika Josephat Isango… (endelea).

Kiongozi mmoja mwandamizi wa BAVICHA makao makuu aliyezungumza na MwanaHALISI Online kwa sharti la kutotajwa jina lake amesema, uamuzi wa wao kwenda Dodoma uko palepale.

“Tumeshaamua kwenda Dodoma na hakuna yeyote anayeweza wa kutuzuia. Uamuzi wetu uko palepale na tutatekeleza kila ambacho tumepanga,” ameeleza.

Mkutano mkuu wa CCM umepangwa kufanyika mkoani Dodoma wiki mbili zijazo. Unatarajiwa kumchagua John Pombe Magufuli, kuwa mwenyekiti wa taifa wa chama hicho.

Msimamo mkali wa kiongozi huyo wa BAVICHA umefuatia uamuzi wa mwenyekiti wa taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, kuzuia vijana wa Chadema kwenda Dodoma kukabiliana na CCM.

Mbowe alitoa kauli hiyo jana Jumapili, kufuatia kuwapo kwa taarifa kuwa jeshi la polisi nchini, limeapa kupambana na viongozi na wafuasi wa Chadema, ikiwa watafika mkoani humo kuzuia mkutano wa CCM.

Chadema kimeamua kuchukua hatua ya kukabiliana na CCM baada ya jeshi la polisi kuzuia mikutano ya ndani ya chama hicho; mikutano ya hadhara na mahafali yaliyopangwa kufanywa na Umoja wa Wanavyuo wa Chadema (CHASO), katika baadhi ya mikoa.

Kauli ya Mbowe imepingwa na baadhi ya vijana katika maeneo mbalimbali, ikiwamo mkoani Arusha, ambako uongozi wa mkoa umekabidhi kwa BAVICHA kiasi cha Sh. 5 milioni kwa ajili ya kwenda Dodoma.

Miongoni mwa mahafali ya Chadema yaliyovurumishwa na polisi, ni pamoja na yale yaliyofanyika mkoani Dodoma ambako mgeni rasmi alikuwa waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.

Mahafali ya Dodoma yalitarajiwa kufanyika katika hoteli ya African Dreems, yaliporomoshwa na polisi kwa kutumia mabomu ya machozi, silaha za moto na gari moja la maji ya kuwasha.

“Upole wa Mbowe na Edward Lowassa, ndiyo uliosababisha tukaibiwa kura na kushindwa kuandamana. Katika hili, hatuko tayari kumsikiliza yeyote,” ameeleza kiongozi huyo.

Anasema, “…kama Mbowe ameshindwa kuongoza chama basi ni vema akaamua kukaa pembeni na kuwacha wenye uwezo na ujasiri wa kutenda.

“Kama anaogopa kuwekwa ndani basi aache kabisa siasa hadi watakapopatikana polisi wapole atarudi kuwa mwenyekiti.”

Akiongea kwa uchungu kiongozi huyo mwandamizi wa Chadema anasema, “tunataka kwenda Dodoma ili azima yetu itimie. Ni lazima polisi na CCM wafahamu kuwa nchi hii siyo mali ya genge la watu wachache. Nasi ni umma ambao unapaswa kutendewa haki.”

Katika mitandao ya kijamii kumesheheni mijadala inayopinga kauli na msimamo wa Mbowe wa kuwazuia BAVICHA kwenda Dodoma na wengine kufikia hatua ya kumshambulia.

Baadhi ya waliojitokeza kupinga uamuzi huo wa Mbowe, ni viongozi wenzake wa Kamati Kuu (CC), Baraza Kuu la taifa (BKT), wabunge, madiwani na viongozi wa mikoa.

Hatua ya polisi kuzuia mikutano ya hadhara ilifuatia kauli ya Magufuli, aliyotangaza zuio la jumla la kufanyika mikutano ya kisiasa ya hadhara na ya ndani na kusema, “wanaotaka kufanya siasa wasubiri hadi mwaka 2020.”

error: Content is protected !!