Sunday , 5 February 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Bavicha wamjibu IGP Sirro kwa hoja
Habari za SiasaTangulizi

Bavicha wamjibu IGP Sirro kwa hoja

John Pambalu, Mwenyekiti wa Bavicha
Spread the love

 

BARAZA la Vijana la chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania- Chadema (Bavicha), limedai kauli ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro, kwamba hawajambambikizia kesi ya ugaidi Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, ni ya kisiasa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne tarehe 3 Agosti 2021, mkoani Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bavicha, John Pambalu wakati akizungumza na wanahabari kuhusu kauli hiyo ya IGP Sirro.

IGP Sirro alitoa kauli hiyo jana Jumatatu, jijini Dar es Salaam, akizungumzia mashtaka ya Mbowe, anayekabiliwa mashtaka ya ugaidi, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Akijibu kauli hiyo, Pambalu amedai si kweli kwamba Jeshi la Polisi halimjambambikizia kesi Mbowe, kwa kuwa lina historia ya kubambikizia kesi wananchi.

Huku akikumbushia agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, kwa jeshi hilo akilitaka lifute kesi za kubambikiza.

“Namkumbusha IGP Sirro, Rais Samia alipoingia madarakani alivionya vyombo vya dola kubambikiza kesi na kesi zaidi ya 100 zilifutwa, za watu waliobambikiziwa.”

“Ni ushahidi tosha kwamba jeshi na vyombo vya dola vimekuwa vikibambikizia watu kesi, ndiyo maana Rais alisema visibambikizie watu kesi,” amesema Pambalu.

Tarehe 18 Mei 2021, Rais Samia akifungua Chuo cha Ushonaji cha Polisi Kurasini, mkoani Dar es Salaam, aliliagiza Jeshi la Polisi, lizifute kesi za kubambikiza ili kupunguza mrundikano wa mahabusu unaosababishwa na kukwama kwa kesi mahakamani, kutokana na kukosekana kwa ushahidi.

Mbali na kukumbusha juu ya kauli hiyo ya Rais Samia, Pambalu amerejea kesi mbalimbali zilizofutwa au maamuzi yake kutenguliwa, kutokana na kuwa za kubambikiza.

Ikiwemo kesi ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, iliyokuwa inamkabili kada wa Chadema, Mdude Nyagali, ambayo Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Mdude alishinda mbele ya Mahakama hiyo baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha madai dhidi ya tuhuma hizo.

Mbali na hayo, Pambalu amehoji kwa nini hadi sasa jeshi hilo halijatoa taarifa dhidi ya hatua ilizochukua, juu ya watu waliohusika katika matukio mbalimbali ikiwemo kuwashambulia viongozi wa Chadema, Tundu Lissu na Mbowe.

Matukio yaliyotajwa na Pambalu, ni kushambuliwa kwa risasi Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu na Mbowe kuvunjwa mguu. Matukio yualiyotokea katika nyakati tofauti jijini Dodoma.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

“Jeshi la Polisi limekuwa likifanya mambo kwa double standard (upendeleo), tangu IGP Sirro alivyoingia madarakani. Lissu alishambuliwa Dodoma, hakuwahi kuwaambia Watanzania nani alimshambulia.”

“Aliposhambuliwa Mbowe Dodoma, akavunjwa mguu wake, jeshi halijawahi kusema linamshikilia nani kutokana na shambulio,” amesema Pambalu.

Pambalu ameongeza “Jeshi la Polisi la IGP Sirro, linaweza likagundua njama za kuuwa viongozi wa Serikali na lisiweze kugundua waliofanya mabaya dhidi ya viongozi wa upinzani. Eti njama anazigundua ila ukimuuliza nani kampiga risasi Lissu, hajui. Ukiuliza nani alimshambulia Mbowe, Sirro hajui.”

Tukio la Lissu kushambuliwa kwa risasi lilitokea tarehe 7 Septemba 2017, jijini Dodoma, hadi sasa Jeshi la Polisi halijatoa taarifa rasmi juu ya washukiwa wa tukio hilo, kwa maelezo kwamba Lissu amegoma kutoa ushirikiano.

Pambalu amemuomba Rais Samia aingilie kati kuhusu sakata hilo, kama alivyofanya katika kesi ya ugaidi iliyokuwa inawakabili Masheikh wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar. Ambao waliachwa huru 2021 baada ya kusota rumande kwa zaidi ya miaka nane.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo aungana na wananchi ujenzi maabara za sekondari

Spread the loveMBUNGE wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, kwa kushirikiana na...

Habari MchanganyikoTangulizi

Haya hapa majina 12 ya familia moja waliofariki kwenye ajali Tanga

Spread the love  MAJINA 12 kati ya 17 ya waliofariki dunia katika...

Habari za Siasa

CCM apiga marufuku wazazi kuwatumia watoto wa kike kwenye mambo ya kimila

Spread the loveKATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Daniel Chongolo...

Habari za Siasa

Ofisi za mabalozi wa mashina zitumike kuwale vijana kimaadili – Chongolo

Spread the loveKATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo ameagiza...

error: Content is protected !!