January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

BAVICHA: Polisi wanadaiwa vitambulisho vya kura

Spread the love

MWENYEKITI wa Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA), Patrobas Katambi amesema wamegundua mipango ya Chama cha Mapinduzi kutaka kupora vitambulisho vya kupigia kura askari polisi kwa maslahi yao. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Tamko hilo la BAVICHA limekuja baada ya kuzagaa malalamiko ya askari polisi kutakiwa kukusanya vitambulisho vya kupigia kura pamoja na majina yao kwa viongozi wao.

Akizungumza na waandishi wa habari, Makao Makuu ya Chadema, Katambi amesema ana ushahidi wa askari ambao walijitokeza kutoa malalamiko juu ya kutakiwa kukusanya vitambulisho vyao pamoja na majina yao.

“Nipo tayari kusimama mahakamani kutoa ushahidi juu ya malalamiko hayo ya polisi. Baada ya kusikia malalamiko hayo, BAVICHA tulichukua hatua za kuwauliza viongozi Serikalini juu ya ukweli huo lakini walikataa. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) walikataa,” amesema Katambi.

Katambi ametaja mikoa ambayo askari walifikwa na tatizo hilo ni Shinyanga, Ruvuma, Morogoro, Dodoma na Arusha. Ambapo askari wa mikoa hiyo walipiga simu na kuuliza juu ya taarifa hizo za ukusanyaji wa vitambulisho.

“Najua hayo yote yanapangwa na CCM ili kuwatishia maaskari wenye mapenzi mema na nchi. Hatuelewi maagizo hayo yalitoka Ikulu au wapi? Maana kila anayeulizwa anakana wakati ushahidi upo,” amesema Katambi.

Pia Katambi amemtaka Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva kutoa ufafanuzi juu ya wanafunzi wa chuo ambao hawakujiandikisha katika daftari la wapiga kura.

“Tunashidwa kuelewa NEC inawaza nini juu ya wanafunzi hao kwani tumefanya uchunguzi na kugundua kuwa wanafunzi wengi hawajajiandikisha kutokana na kupishana na ratiba ya NEC lakini hakuna tamko lolote hadi sasa,” amesema Katambi.

Ameongeza, NEC wanatakiwa kuongeza siku za kuhakiki majina ya waliojiandikisha kupiga kura kwani muda wa siku tano zilizopangwa hazitoshikutokana na wingi wa watu.

error: Content is protected !!