April 14, 2021

Uhuru hauna Mipaka

BAVICHA ni toka ingia

Spread the love

PATRICK Ole Sosopi, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anayemaliza muda wake, amesema hana mpango wa kugombea tena nafasi hiyo. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Ole Sosopi ametoa msimamo huo leo tarehe 28 Novemba 2019, alipozungumza na MwanaHALISI ONLINE, kwa njia ya simu.

Amesema, ameona ni busara kuwapa nafasi vijana wa chama hicho, kugombea uenyekiti wa Bavicha.

“Sitagombea uenyekiti wa BAVICHA, licha ya kwamba Katiba inaniruhusu, lakini ni zamu ya watu wengine wapya, mimi nimeitumikia kwa uaminifu. Naona ni busara niwape nafasi wengine, waweze kupikwa sababu Bavicha ni tanuru la kupika viongozi wa chama,” ameeleza Ole Sosopi.

Ole Sosopi amesema kwa sasa anahitaji kuitumikia Chadema katika ngazi ya kitaifa, iwapo atapata ridhaa ya chama hicho.

“Ni wakati wa kukitumikia chama katika nafasi nyingine, sababu uchaguzi wa kitaifa bado unaendelea. Nitakapo jiridhisha nitatangaza baadae nitagombea wapi, lakini kwa sasa ni mapema mno,” amesema Ole Sosopi.

Wakati Ole Sosopi akitoa msimamo huo, Mdude Nyagali, Ofisa Mafunzo wa Chadema Kanda ya Nyasa, ametangaza kugombea nafasi hiyo.

Mdude ameuambia mtandao wa MwanaHALISI ONLINE kuwa, leo natarajia kurudisha fomu ya kugombea nafasi hiyo, katika Ofisi za Mbaraza ya Chadema zilizoko Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

“Mimi nagombea, nimetia nia na fomu nilichukua, kwa sasa niko njiani naelekea kwenye ofisi za chama kurudisha fomu yangu. Nafikiri itakuwa saa saba mchana,” ameeleza Mdude.

Ole Sosopi amehudumu katika nafasi ya Unyekiti wa Bavicha kuanzia mwishoni mwa mwaka 2016, baada ya Patrobas Katambi, aliyekuwa mwenyekiti wa baraza hilo, kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kabla ya hapo, Ole Sosopi alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, ambapo alichaguliwa kushika nafasi hiyo, mwaka 2014.

error: Content is protected !!