August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bavicha haturudi nyuma- Sosopi

Spread the love

 

PATRICK Ole Sosopi, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) amesema, kamwe vijana wa chama hicho hawatarudi nyuma katika kupigania demokrasia inayominywa na kukandamizwa hapa nchini, anaandika Charles William.

Hivi karibuni Sosopi alikamatwa na Jeshi la Polisi na kusafirishwa kutoka mkoani Iringa mpaka jijini Dar es Salaam, kwa tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi katika hafla ya mahafali ya wanafunzi wa vyuo vikuu ambao ni wanachama wa Chadema.

Akizungumzia sakata hilo pamoja na hali ya kisiasa hapa nchini, makamu huyo wa Bavicha taifa amesema, Jeshi la Polisi linaendelea kumsumbua kwa kumwita mara kwa mara katika Makao Makuu yake pasipo kumfikisha mahakamani.

“Tangu nikamatwe na kuachiwa, natakiwa kuripoti Makao Makuu ya Polisi. Nilifanya hivyo 6 Julai na 18 Julai mwaka huu na pia wanataka niende tena tarehe 1 Agosti jambo ambalo ni usumbufu usio na maana, kama kuna kosa kwanini hawanipeleki mahakamani?” amehoji Sosopi.

Sosopi amesema, yeye kama kiongozi wa Bavicha anashindwa kufanya ziara za kikazi na shughuli zake binafsi za kujiingizia kipato kwasababu ya wito wa mara kwa mara wa polisi jijini Dar es Salaam huku akilitaka jeshi hilo lichague kumwacha huru au kumfikisha kortini.

“Nalitaka Jeshi la Polisi liache kufanya kazi kwa maagizo ya wanasiasa na badala yake lizingatie weledi.

“Lisijihusishe na propaganda za kisiasa, lifuate taaluma ili lisiendelee kupoteza heshima na mvuto mbele ya umma,” amesema Sosopi.

Sosopi ameyasema hayo, alipozungumza na Mwanahalisi Online ikiwa ni siku tatu kabla ya Kikao cha Kamati ya Utendaji ya Bavicha Taifa kukutana jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuibuka na kile kinachotajwa ‘mbinu mpya’ ya kukabiliana na wakandamiza demokrasia.

“Bavicha hatuna uoga, kama wanadhani watatutisha kwa kutufungulia kesi kila mahali basi wajue kuwa kamwe hatutarudi nyuma, tutawaongoza vijana wote nchini kuwakabili wakandamiza demokrasia likiwemo jeshi la polisi na serikali.” Amesisitiza Sosopi.

Viongozi wengine wa juu ya BAVICHA akiwemo Patrobas Katambi mwenyekiti taifa na Julius Mwita ambaye ni Katibu wanakabiliwa na kesi uchochezi mkoani Dodoma wakidaiwa kuvaa fulana zenye maneno ya kichochezi; “Mwalimu Nyerere: demokrasia inanyongwa.”

20 Julai Mwaka huu, kamati ya utendaji ya BAVICHA taifa itafanya kikao ambacho pia mwenyekiti wa Chadema taifa Freeman Mbowe ambaye hivi karibuni aliwaomba vijana hao kusitisha safari ya kwenda mkoani Dodoma 23 Julai kuzuia mkutano mkuu wa CCM amealikwa kushiriki.

 

error: Content is protected !!