November 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bashe: Matokeo ya uwekezeji kilimo hayatokei siku moja

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe

Spread the love

 

WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe amewataka Watanzania wasidhani kwamba matokeo ya jitihada za Serikali kuboresha sekta ya kilimo yanatokea siku moja bali ni uwekezaji wa muda mrefu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Amesema kama hawatofanya mabadiliko ya kilimo katika kipindi hiki basi wasahau kwani wana rais ambaye ana utashi wa kisiasa ana utayari wa kuweka fedha ili kuondoa matatizo ya sekta hiyo.

Bashe ametoa kauli hiyo leo tarehe 22 Novemba, Kondoa mkoani Dodoma baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumkaribisha kusalimu wananchi wakati akiwa kwenye safari ya kuelekea mikoa ya Manyara na Arusha.

Amesema bajeti wizara hiyo imeongezeka huku Sh bilioni 150 zikitengwa kwa ajili ya ruzuku ya mbolea na Sh bilioni 369 kujanga miundombinu ya umwagiliaji.

Aidha, amewatahadharisha wakulima kutouza namna zao za siri kwa ajili ya kupewa mbolea ya ruzuku kwani katika mkoa wa Kigoma zaidi ya wakulima 20 wamekamatwa kwa kuuza namna hizo za siri kwa wafanyabiashara wakanunue mbolea kwa niaba yao.

Rais Samia Suluhu Hassan

“Leo wapo ndani, msiuze namba zenu za siri kwa sababu ruzuku imetolewa kwa ajili ya ninyi wakulima ili muende shambani mkafanye uzalishaji, mkapunguze gharama za uzalishaji na serikali imewaruhusu kuuza mazao yenu popote msiwe na hofu.

“Serikali inakupa ruzuku inataka ile mbolea ya inayouzwa Sh 140,000 uipate kwa Sh 70,000 unachotakiwa kwa kuwa umesajiliwa na una namba ya siri, wewe ndio ukanunue ile mbolea kupeleka shambani kwako,” amesema.

Aidha, amesema kutokana na ukame, serikali imeamua kuanzisha miradi ya umwagiliaji kwani kwa muda mrefu matatizo ya kilimo yalikuwa yanatatuliwa kwa matukio lakini serikali ya awamu ya sita imeamua kuyatatua matatizo ya msingi kwa kuwekeza kwa muda mrefu.

“Tatizo la mbegu, serikali inatoa ruzuku ya mbegu. Lakini baada ya miaka mitatu taifa litakuwa linajitegemea kwenye mbegu kwa sababu mwaka huu tumeanza kujenga miundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba ambayo toka tupate uhuru hayajawahi kujengewa miundombinu ya uwagiliaji,” amesema.

Halmashauri 41 zagawiwa chakula
Aidha, amewahakikishia Watanzania kuwa hakuna Mtanzania atakayekufa kwa njaa kwani serikali ina chakula cha kutosha.

“Hivi sasa kupitia wizara, halmashauri zinaonesha na kutuletea taarifa pale ambapo bei ya mahindi inakuwa imepanda sana serikali inapeleka chakula na kuuza kwa bei ya chini ili wananchi waweze kununua.

“Mpaka halmashauri 41 tumeshazipelekea chakula na serikali tunafungua duka chini ya maelekezo ya halmashauri tunauza chakula kwa mwananchi mmoja mmoja kwa bei ya chini sio kuwauzia wafanyabiashara,” amesema.

Amesema kuanzia Disemba mwaka huu Serikali itatoa huduma bure kwa kugawa vipima afya ya udongo ili kutambua aina ya mazao yanayopaswa na mbolea inayopaswa kutumia katika udongo husika ikiwamo mkoa wa Dodoma ambao wakulima wake wana utamaduni wa kutotumia mbolea.

Amesema serikali inajenga maghala kwa ajili ya wakulima kuhifadhi mazao badala ya kwenda kuhifadhi mtaani na ambako wanaenda kupata matatizo ya sumu kuvu.

“Huduma hii itakuwa kwa wakulima vijijini, tunajenga maghala zaidi ya 70 katika halmashauri zenu, halmashauri ya Kondoa tunajenga ghala moja la bilioni 1.2,” amesema.

error: Content is protected !!