January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bashe kufuatilia mahakama ya mafisadi

Spread the love

MGOMBEA ubunge jimbo la Nzega mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hussein Bashe amesema akiingia bungeni atafuatilia kwa karibu uanzishwaji wa mahakama maalum kwa ajili ya kuwashughulikia “mafisadi na majizi.” Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Ahadi ya kuanzisha mahakama maalum kwa ajili ya kuwashughulikia “mafisadi na majizi” ameitoa mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dk. John Magufuli kama hatua ya kukomesha utamaduni wa kufisidi raslimali za nchi uliokithiri serikalini.

Bashe akihutubia mkutano wa kampeni ya Dk. Magufuli mkoani Tabora leo, amesema kuwa atakapokuwa mbunge atahakikisha anafuatilia kuona ahadi hiyo inatekelezwa kwa vitendo.

“Umefika wakati lazima Watanzania waache kupenda porojo, ahadi za porojo hazitakiwi sasa, wananchi nitasimamia kuhakikisha mahakama ya kushughulikia mafisadi na majizi inatekelezwa,” amesema.

“Nitafuatilia kuona ahadi ya Dk. Magufuli ya kuanzishwa kwa mahakama maalum kwa ajili ya mafisadi na majizi inatekelezwa kwa vitendo,” amesema Bashe, kijana anayegombea ubunge tena baada ya jitihada zake kugombea uchaguzi uliopita kukwamishwa na chama hicho kilichomtema kwa madai uraia wake ulikuwa na utata.

Katika uchaguzi mkuu wa 2010, Bashe aliwania kuomba ateuliwe na CCM lakini Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama (NEC-CCM) haikumteua kwa sababu ya walichosema, kuna tatizo katika uraia wake.

Akiwa ni kada anayechukuliwa kama mtu wa karibu na waziri mkuu aliyejiuzulu mwaka 2008 kwa shinikizo la Bunge, Edward Lowassa, Bashe amesema anataka kuona ahadi hiyo ya Dk. Magufuli inatekelezwa.

Dk. Magufuli amekuwa akieleza Watanzania kwingi anakopita kuomba ridhaa ya kuongoza taifa katika uchaguzi wa Oktoba 25, kwamba kwa sababu serikali iliyopo imekuwa ikikabiliwa na ufisadi mkubwa, yeye hatakuwa na muhali.

Dk. Magufuli amesema iwapo atachaguliwa kuongoza taifa, serikali atakayoiunda itakuwa ya kazi na kuonya asiyekuwa tayari kufanya kazi kwa kasi, apumzike mapema.

error: Content is protected !!