FC Barecelona imejikuta ikipoteza pointi tatu muhimu, katika Uwanja wake wa nyumbani “Camp Nou” kwa kukubali kipigo cha 2-1 kutoka kwa Granada. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Barcelona imepokea kipigo hicho jana usiku Alhamisi, tarehe 29 Aprili 2021, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Hispani (La Liga).
Kipigo hicho, kimewafanya kushindwa kupanda kileleni mwa ligi hiyo inayoongozwa na Atletico Madrid yenye pointi 73 na Barcelona iko nafasi ya tatu ikiwa na pointi 71.
Real Madrid nayo ina pointi 71 na timu zote, zimecheza michezo 33 na imesalia mitano kuhitimisha ligi hiyo.
Sevilla iko nafasi ya nne, ikiwa na pointi 70.
Endapo ingeshinda, Barcelona ingefikisha pointi 74. Hata hivyo, ilijikuta ikipokea kipigo hicho na kuwafanya Granada kufikisha pointi 45 ikiwa nafasi ya nane ya msimamo wa ligi hiyo.

Lionel Messi, aliipeleka Barcelona mapumziko ikiongoza 1-0, goli alilolifunga dakika ya 23.
Kipindi cha pili kilipoanza, Granada iliwachukua dakika 18 kusawazisha kupitia kwa Darwins Machis ikiwa ni dakika ya 63.
Dakika 16 baadaye, Jorge Molina aliifungia goli la ushindi Granada ikiwa ni dakika 79 na kuwabakisha Barcelona kwenye nafasi yao ya tatu.
Wakati ligi hiyo ikiwa imebakisha michezo mitano kila timu, timu nne, za Atletico Madrid, Real Madrid, Barcelona na Sevilla, yeyote kati yake, anaweza kutwaa ubingwa huo, kutokana na pointi walizonazo kila mmoja.
Leave a comment